Thursday, 22 February 2018

NEC YATOA UFAFANUZI JUU YA MUITIKO MDOGO WA WAPIGA KURA

NEC Yafunguka Juu ya Mwitikio Mdogo wa Wananchi Katika Kupiga Kura
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imejibu hoja mbalimbali zinazotolewa na wadau kuhusu sababu zinazochangia mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kupiga kura tofauti na idadi ya watu waliojiandikisha.

Ufafanuzi huo unatokana na idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha uliofanyika Februari 17 pamoja na chaguzi nyingine za hivi karibuni za ubunge na udiwani.

Katika Jimbo la Kinondoni kati ya wapiga kura 264,066 waliojiandikisha ni wapiga kura 45,454 tu waliofika kupiga kura, huku Siha kati ya waliojiandikisha 55,313 waliopiga kura ni 32,277.

Katika uchaguzi mdogo wa majimbo ya Kalenga na Chalinze uliofanyika Machi 16, 2014, kati ya waliojiandikisha kupiga kura 71,964 ni 29,541 tu walijitokeza kupiga kura huku Chalinze kati ya 92,000 walioandikishwa waliopiga kura walikuwa 24,422.

Pia, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ni wapigakura milioni nane pekee waliopiga kura kati ya milioni 21 waliojiandikisha huku mwaka 2015, kati ya wapiga kura milioni 23.2 walioandikishwa na waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 15.6.

Jana, Naibu Katibu Uendeshaji Uchaguzi wa NEC, Irene Kadushi alijibu hoja mbalimbali za wadau akisema mwitikio wa wapiga kura wakati wa chaguzi ndogo hutofautiana na wakati wa uchaguzi mkuu na kitendo cha watu kuhama chama kimoja na kisha kuruhusiwa kugombea nafasi ile ile imechangia idadi ndogo ya wapigakura kwenye uchaguzi mdogo wa Februari 17. “Miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto ya fedha katika kutoa elimu ya mpiga kura, lakini tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa kutosha na sasa elimu ya mpiga kura ni endelevu. Hakuna taasisi yoyote inayoiingilia NEC katika utendaji wake ikiwemo Serikali ambayo jukumu lake huishia kwenye kuipatia tume fedha kwa ajili ya shughuli zake,” alisema.

Bosi huyo wa uchaguzi wa NEC alisema muundo wa tume hiyo unachangia wananchi kuwa na mtazamo kuwa wateule wa Serikali wanaosimamia uchaguzi kwenye ngazi za chini wanakipendelea chama tawala.

“Hii imepelekea (sababisha) sisi kuomba tupatiwe ofisi kwenye kanda mbalimbali hapa nchini jambo litakalotusaidia pia katika utunzaji wa vifaa vyetu vya kazi. Pia, tunataka tuwe na uwezo wa kuajiri wafanyakazi hasa wasimamizi wa uchaguzi hali itakayoiongezea tume kuaminika kwake,” alisema na kuongeza.

“Kikubwa ni watu waongeze uaminifu wao kwa tume ambayo imekuwa ikifanya kazi kubwa, kwani hata nchi ambazo tume zake zinaonekana ziko huru na haki bado zinalalamikiwa kwa mambo kadha wa kadha.”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search