Friday, 2 February 2018

Rais Magufuli Amtaka Jaji Mkuu Kuwachukulia Hatua Majaji Wanaenda Ughaibuni Kula Bata

Rais Magufuli Amtaka Jaji Mkuu Kuwachukulia Hatua Majaji Wanaenda Ughaibuni Kula Bata
Rais John Magufuli amemtaka Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kuwachunguza majaji wote ambao wamekuwa wakisafiri wakati wa likizo zao kwenda ughaibuni ‘kula bata.’

Pia, Rais Magufuli amesikitishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju akisema kwa miezi tisa wameshindwa kuandaa kanuni za msaada wa kisheria na kuagiza zikamilike mwezi huu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Sheria, Rais Magufuli alisema kuna watumishi wachache wasiokuwa waadilifu ambao wanachafua vyombo vya kutoa haki na “Sitaki kuona hili likiendelea kwa wale wasiokuwa na uadilifu.”

Kuhusu majaji hao, Rais Magufuli alisema kumekuwapo na baadhi yao ambao kila wanapopata likizo wanasafiri kwenda nje ya nchi kwa siku 28 na yeye ndiye anayetoa vibali huku anayegharamikia usafiri na kuishi hoteli nzuri akiwa hajulikani.

Alisema aliwahi kumuuliza Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma kuhusu majaji hao wanaokwenda huko kwamba ni nani anayegharamia huku akidokeza kuwa anazo taarifa nyingi.

“Jaji Mkuu, hili ni swali najiuliza sana, wanapokwenda na familia zao wanaishi hoteli nzuri, mishahara ya majaji naijua kama wa kwangu tu, Jaji Mkuu kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo wewe ni mwenyekiti chunguza vibali vyao, kwa nini iwe kina fulani fulani tu,” alihoji Rais Magufuli.

Rais alipongeza Profesa Juma kwa kuwachukulia hatua watumishi 112 wa Idara ya Mahakama ambao awali, jaji mkuu alieleza kwamba baadhi yao walifukuzwa kazi na wengine kustaafishwa akisema uamuzi huo unajenga taswira nzuri ya chombo cha utoaji haki.

Hata hivyo, alisema licha ya pongezi alizozitoa, usimamizi wa sheria na utoaji wa haki bado una changamoto kwani wapo watumishi wachache wasio waadilifu ambao vitendo vyao vinachafua mhimili huo.

“Wapo wachache, wachache, nasema wachache wanaochafua taswira yetu ambao wanatoa hukumu zinazopendelea watu, kuchelewesha hukumu, kuchelewa kuandika hukumu na kati yao ni hao 112 tulioelezwa na Jaji Mkuu waliofukizwa au kustaafishwa,” alisema Rais Magufuli na kuongeza,

“27 walistaafishwa kwa masilahi ya wananchi na walikuwa mahakimu na wote walipopelekwa mahakamani walishinda, yaani kesi ya ngedere unaipeleka kwa nyani unategemea nini? Mahakimu 14 walifukuzwa kazi, 67 watumishi wa kawaida nao walifukuzwa kazi.”

Kuhusu hilo, Jaji Mkuu Profesa Juma alisema kati mwaka 2016/17, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilisikiliza malalamiko ya kimaadili 143 na kati ya waliofukuzwa au kustafishwa ni 112 na 17 walirudishwa kazini.

“Hatutamwonea mtumishi lakini hatutamvumilia mtu anayetupaka matope sisi kama Mahakama,” alisema Jaji Mkuu.

Akizungumza kwa msisitizo, Rais Magufuli alisema “Wito wangu kwa vyombo vingine IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi- Saimon Sirro) yupo hapa, Mkuu wa Magereza, Takukuru na vyombo vingine vinavyotoa haki muige mfano wa Profesa Juma.

Ningefurahi kuona “IGP anatoa majina ya polisi wanaochelewesha upelelezi. Unakuta mtu ameshikwa na dawa za kulevya unaambiwa upelelezi bado, Magereza watu wanaoingiza simu au dawa za kulevya gerezani na DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) ambaye hata hivyo, hana uwezo wa kuhamisha watumishi na ndio maana wengine wanaletwa kwangu.”

Rais Magufuli alisema hayo yamesababisha baadhi ya kesi kushindwa na kudokeza kuwa ameshajua wapi tatizo lilipo na kwamba atachukua hatua haraka.

“Majaji mnisamehe. Sitalalamika tena, nishajifunza, najua wapi tunakosea, mwaka jana nililalamika, mwaka huu sitalalamika, najua jinsi ya kufanya na wala mwezi huu hautaisha,” alisema Rais Magufuli.

Profesa Kabudi, AG Masaju

Rais Magufuli akijibu ombi la Jaji Mkuu Profesa Juma la mkwamo wa utekelezaji wa Mahakama inayohama kutokana na kanuni kutokukamilika, alisema inasikitisha wale anaowateua wanashindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo licha ya kulipwa mishahara.

“Bunge limepitisha, mimi nimesaini lakini Waziri wa Katiba na Sheria tena Profesa (Kabudi), tatizo huyu mtani wangu, lakini mimi ndivyo nilivyo kusema hadharani, Mwanasheria Mkuu (Masaju), Naibu Mwanasheria Mkuu (Gerson Mdeme) wote wapo, wanakula mishahara, magari ya kiyoyozi wanayo lakini miezi tisa wameshindwa kuandaa kanuni,” alisema Rais Magufuli.

“Wakati mwingine na mimi najitathimini nawachaguaje chaguaje hawa. Nataka mwezi huu kanuni ziwe zimekamilika kwani wakati mwingine majaji na Mahakama wanalalamikiwa bure kuchelewesha haki kwa makosa ambayo sio ya kwao.”

Profesa Juma alisema Mahakam inayotembea (katika gari) imeshindwa kuanza kazi kutokana na kutukuwapo kwa kanuni hivyo kuiomba Wizara ya Katiba na Sheria kuzifanyia kazi ili huduma hiyo ianze kutolewa.

Kuhusu vitendo vya rushwa, Rais alisema vipo na “Nina taarifa nyingi kwelikweli, rushwa haifichiki na Jaji Mkuu hao majaji wanaokwenda Ulaya fuatilia vibali vyao.”

Matumizi ya Tehama

Awali, Profesa Juma alisema umuhimu wa Mahakama lazima upewe kipaumbele na kwa kutumia Siku ya Sheria, watafakari walipotoka, walipo na wanapokwenda hasa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Alisema Mahakama imejiwekea malengo ya kuongeza kasi, uwazi na uadilifu na hawataki kusikia shauri la mtu halijulikani lilipo, kesi yake ni lini na nani atalisikiliza akisisitiza Tehama inakuja kuweka uwazi zaidi na kuondoa unjanjaunjanja.

“Wananchi wa Tanzania, watarajie huduma bora za uendeshaji wa kesi, uwazi na huona hukumu kwani Tehama itarahisisha yote haya na sisi majaji, mahakimu na watendaji wa Mahakama tubadili fikra zetu na kuijua Tehama kwani karne hii inahitaji kwenda na wakati,” alisema Profesa Juma.

Alisema utaratibu unafanyika ili kukamilisha mfumo wa menejimenti za kesi ambao utatumika kulipa ada na uendeshaji wa kesi kwa masafa ya mbali.

Jaji Mkuu alizungumzia upungufu wa majaji akisema kwa sasa wapo 62 pekee ambao kwa mwaka kila mmoja anakuwa na majalada 535 badala ya 225 jambo ambalo linawasababishia mzigo mzito.

“Huu ni mzigo mkubwa sana na uko nje ya makubaliano kwamba kila jaji amalize majalada 225 lakini kwa idadi hii ni mzigo mkubwa sana,” alisema Profesa Juma

Alisema mpaka sasa ni mikoa 14 kati 26 pekee yenye Mahakama Kuu na kusema malengo ni kuwa na Mahakama Kuu katika mikoa 22 ifikapo mwaka 2020.

TLS yalia na Mahakama

Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi mbali na kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais Magufuli alitoa wito kwa majaji kuhakikisha wanasimamia haki ipasavyo.

Alisema Mahakama panafaa kuwa mahali palipotukuka kwani ndipo pekee ambako kunapokuwa na migogoro na watu wanapoililia sheria wanakwenda bila kujali aina ya mtu.

“Tusiitumie Mahakama kama majaribio, maabara au jumba la kamari. Majaji msiitumie hata mara moja kwani mnalindwa kisheria na msimamie hilo ili Mahakama isionekane ya ajabu ajabu.”

Awali, Mdeme alisema utoaji haki unahitaji ushirikiano kutoka wa wadau mbalimbali na ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekuwa ikifanya hivyo kwa masilahi ya Taifa na wananchi.

Mdeme alisema mfumo wa Tehema utapunguza gharama, urasimu, kuwahisha utoaji wa haki na utawaanika watumishi wasio waaminifu hivyo kuhimiza kila mmoja kujifunza na kuutumia. 

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search