Wednesday, 21 February 2018

SERIKALI IMESEMA ITAANGALIA VITU VYA MSINGI KWENYE KUGHARAMIA MAZISHI YA AKWILINA

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo amesema, serikali itaangalia vitu vya msingi vya kugharamia kwa ajili ya mazishi ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), cha jijini Dar es Salaam.

Msichana huyo, Akwilina Maftah (22) alikufa kwa kupigwa risasi Februari 16 mwaka huu, Kinondoni jijini humo.

Familia ya Akwilina, imekabidhi Serikalini bajeti ya Sh milioni 80 ya mazishi.

“Wao wameandaa bajeti hiyo lakini na sisi kama Serikali tuna vitu vya msingi vya kugharamia ambavyo ni kama chakula, usafiri, jeneza na vingine,” amesema Dk Akwilapo.

Familia ya marehemu jana ilikabidhi bajeti hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo kwa utekelezaji kama ambavyo serikali iliahidi kugharamia msiba huo.

Msemaji wa familia, Festo Kavishe aliliambia gazeti hili jana kuwa familia imeandaa bajeti hiyo kwa ajili ya kufanikisha mazishi na kuikabidhi kwa serikali na kwamba watashukuru endapo watapatiwa fedha zote kama walivyoomba.

“Ni kama mtu umebeba ndoo mbili za maji, mtu akija akakupokea ndoo moja utashukuru, akikupokea ndoo zote mbili utashukuru zaidi, kwa hiyo na sisi hatuna namna serikali itakavyoamua kusaidia sawa,” alisema.

Alisema katika msiba huo watu wanaotarajiwa kusafiri na mwili kwenda kwenye maziko Rombo mkoani Kilimanjaro ni 300 ambao ni ndugu, jamaa na wanachuo waliokuwa wakisoma na Akwilina.

Chanzo: Habari leo

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search