Tuesday, 6 February 2018

UTEUZI WA DR. ADELARDUS KILANGI KUWA AG


Ezekiel Kamwaga
Maoni yangu
Jana usiku Rais John Magufuli amemteua Dk. Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali.
Nadhani ni uteuzi unaosisimua. CV ya AG mpya imeshiba na kwa bahati nzuri ni mtu ambaye haogopi kuweka maoni yake hadharani.
Mimi ni mmoja wa watu wanaoamini kwamba nafasi ya AG ni ya kisiasa pia na ndiyo maana bungeni ni mtu muhimu.
Nasubiri kuona ladha yake wakati atakapoanza kutekeleza majukumu yake bungeni.
Kwa maoni yangu, Andrew Chenge, ndiye alikuwa AG wa mwisho ambaye kila aliposimama kuzungumza bungeni ilibidi umsikilize.
Frederick Werema hakuwa mbaya lakini alikuwa na jazba. Ndiyo sababu hakusita kumwita mbunge "tumbili". Hutaraji AG kutumia lugha ya namna hii.
George Masaju ni mwanasheria mzuri lakini ule " Uanasiasa" wa AG ulimpa shida kidogo. Hapa, ilikuwa sawa na kutaka kutumia ufunguo wenye umbo la mraba kutaka kufungua kitasa chenye umbo la duara.
Wakti utaamua namna Kilangi atakavyochambuliwa baadaye.
# Mazuri
Rais kampa nafasi mtu ambaye wasifu wake hauna shaka. Hapa, amemweka samaki kwenye maji.
Pia, Rais ameonyesha kwamba bado anataka kulifanyia kazi eneo la rasilimali zetu. Hajapoteza focus kwenye hilo.
Kilangi ni mbobezi wa Sheria za Kimataifa na mjuzi wa masuala ya rasilimali. Katika wakati huu ambapo nchi bado inasukumana na wakubwa hawa, Kilangi ndiyo aina ya mtu ambaye anafaa.
Nimezungumza na Godwin Ngwilimi, mmoja wa viongozi wa TLS na Alumni wa Sekondari ya Sengerema kama alivyo Kilangi na amemuelezea AG mpya kama mtu mwenye akili, mzalendo, mbobezi, muungwana na mwenye msimamo. Hizi ni sifa za mtu anayetosha.
# Mapungufu
Wakosoaji wa Rais Magufuli wamekuwa wakizungumza kuhusu asivyozingatia mgawanyo wa kijinsia, kidini na kikanda katika utekelezaji wa majukumu yake.
Uteuzi huu, unatoa fursa ya kuibuka tena kwa wakosoaji wake. Labda nieleze kwa mifano kidogo.
Rais ameteua Jaji Mkuu kutoka Kanda ya Ziwa. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ametokea hukohuko, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) wanatokea Kanda ya Ziwa pia ingawa hawa hawakuteuliwa na Rais Magufuli.
Kilangi anatokea Kanda ya Ziwa pia. Nimetaja taasisi hizi kwa sababu zote zinahusika na utoaji wa haki.
Hii inanikumbusha kuhusu rafiki yangu Jamal Malinzi. Siku moja tulizungumza tukiwa Maputo na aliniuliza maoni yangu kuhusu namna watu wanavyomuna huko nje. Nikamwambia watu wanasema unapendelea sana Kagera. Akaniambia atarekebisha hilo.
Siku chache baadaye, aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria wa TFF, Evodius Mtawala, akajiuzulu wadhifa wake huo. Mtu wa Kagera huyu. Nikajua Malinzi kapata fursa ya kurekebisha mambo.
Akamteua Emmanuel Muganyizi (Muga) kushika wadhifa huo. Niliposikia nilicheka tu.
Rais Magufuli alikuwa na fursa ya kumteua mwanamama kwenye wadhifa huo ili kubadili upepo na kuweka historia mpya maana hakuna mwanamama aliyewahi kushika wadhifa huo.
Alikuwa na uwezo wa kumteua pia Mtanzania mwingine mwenye sifa kutoka eneo lingine la Tanzania lakini yeye kaamua vinginevyo.
Wachina wanasema rangi ya paka si muhimu ali mradi anakamata panya.
Labda tatizo letu kama nchi kwa sasa ni kuwa na paka wanaokamata panya wengi na baadaye tatizo likiisha tutaanza kujali kuhusu rangi.
Mpira huu umerushwa kwa AG mpya. Namtakia kila la kheri.
Ezekiel Kamwaga
Dar es Salaam
Februari 2018

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search