Friday, 16 February 2018

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametangaza kutaifishwa kwa meli iliyofanya Uvuvi haramu

Related image
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametangaza kutaifishwa kwa meli ya Kampuni ya Buah Naga One ya nchini Malaysia, baada ya mmiliki wa meli hiyo kukaidi amri halali ya Serikali iliyomtaka kulipa faini ya Dola za Marekani 350,000 sawa na Sh milioni 770 ndani ya siku saba.

Ni baada ya meli hiyo kubainika kukiuka Kanuni ya 66 ya Kanuni za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na Kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 1998 na Marekebisho yake ya Mwaka 2007.

Meli hiyo ilifanyiwa ukaguzi na Kikosi Maalum cha Doria, Januari 25, mwaka huu wakati ikiendelea na shughuli za uvuvi katika bahari kuu kati ya Mkoa Lindi na Mtwara na kukutwa na mapezi na mikia ya samaki aina ya papa 30 bila kuwepo miili yake, huku ikikutwa na samaki wasiotarajiwa (by catch) tani nne kinyume cha sheria.

Waziri Mpina aliagiza pia meli hiyo, kuondolewa Bandari ya Mtwara na kuwasilishwa Bandari ya Dar es Salaam kwa hatua zaidi. Kutokana na uamuzi huo wa serikali, Waziri Mpina alimugiza Katibu Mkuu Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Yohana Budeba kuharakisha mchakato wa kuomba kibali cha Mahakama ili kuruhusu meli hiyo kutaifishwa.

Mbali ya meli, aliagiza pia samaki tani 42 pamoja na samaki wasiotarajiwa tani nne waliokuwemo kwenye meli hiyo, wauzwe kwa mnada na mapato yaingie serikalini.

Akizungumza baada ya kukagua meli ya uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China, iliyotia nanga katika Bandari ya Dar eS Salaam kwa ajili ya ukaguzi, Mpina aliagiza pia vyombo vya dola kuisaka na kuichukulia hatua kali za kisheria meli ya Kampuni ya ‘Tai Hong No. 1’ ambayo ilikaguliwa na kukutwa na mikia ya papa 44 bila kuwa na miili yake kinyume cha sheria za uvuvi.

Alisema nahodha wa meli hiyo, alionesha upinzani mkubwa kabla hajakaguliwa, ambapo alikutwa na makosa mengi ya uchafuzi wa mazingira huku meli hiyo ikitoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Katika hatua nyingine, Waziri Mpina alisema jumla ya meli 24 zilipewa leseni ya uvuvi wa Bahari Kuu, ambapo hadi sasa ni meli nane tu ndizo zilizokaguliwa huku meli nyingine 16 zikitoroshwa na kukimbia kutoka katika ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu kuelekea maji ya kimataifa, sehemu ambayo meli hizo zisingiweza kukamatwa.

"Meli hizo 16 zilizotoroshwa na kukimbia kabla ya kukaguliwa, zifuatiliwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu sheria, kwa kuwa taarifa zao zote zipo na ikithibitika kuna watumishi wa wizara yangu wamehusika na hujuma hiyo, watakuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Mpina.

Alisema baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, mwaka 2016 ilifanya marekebisho ya Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 na kuweka vifungu vipya, ambavyo vitasaidia serikali kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi ili kuliwezesha Taifa kunufaika zaidi na rasilimali hizo.

Mpina alivitaja vifungu hivyo kuwa ni pamoja na kila meli kukaguliwa kabla ya kuanza kuvua na baada ya kumaliza kuvua ;huku sharti la kila meli ya uvuvi kupakia asilimia 10 ya mabaharia walioko kwenye meli hizo, liliwekwa na kuwezesha jumla ya mabaharia 44 wa Tanzania kuingia katika meli hizo na kupata ujuzi wa uvuvi wa bahari kuu.

Sharti lingine ni kushusha samaki wasiotarajiwa na kukabidhiwa katika Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), ambapo jumla ya tani 48 zilishushwa na kuuzwa, pia kutoza mrabaha wa dola za Marekani 0.4 kwa kila kilo ya samaki wanaovuliwa ukanda huo.

Mpina alilisisitiza msimamo wa Serikali wa kukagua meli zote, zinazokuja kuvua katika ukanda wa bahari kuu ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo, kwani kwa miaka mingi Tanzania iligeuzwa 'shamba la bibi' kwa kila mtu kuja kuvua na kukimbia na rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Alipongeza hatua ya meli ya uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China, iliyotia nanga katika Bandari ya Dar eS Salaam kwa ajili ya ukaguzi. Alitaka huo uwe mfano wa kuigwa kwa meli zote kufanya hivyo na kusisitiza kuwa Serikali haina ugomvi na wawekezaji kwenye Sekta ya Uvuvi wanaotii sheria za nchi.

Dk Budeba alisema rasilimali za uvuvi zilizoko majini ni kubwa, hivyo serikali itaendelea kufanya juhudi zote kuhakikisha zinalindwa na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

Alisema maagizo na maelekezo yote, yaliyotolewa na Waziri Mpina atayasimamia kikamilifu, kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati. Aliwaonya watumishi wa wizara yake, wanaosimamia sekta ya uvuvi kutojihusisha na vitendo udanganyifu katika ukaguzi wa meli hizo ili serikali iweze kupata mapato stahiki yatokanayo na utajiri huo.

Chanzo: Habari leo

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search