Thursday, 8 March 2018

ABDUL NONDO ALIYERIPOTIWA KUTOWEKA APATIKANA

Image may contain: 2 people, people sitting and beard
Baada ya kelele za wadau mbalimbali hatimaye kijana Abdul Nondo amepatikana huko Mafinga mkoani Iringa usiku huu. Abdul anadai kutekwa (na watu wasiojulikana) jana majira ya saa 6 usiku maeneo ya Mwengi jijini Dar es Salaam, na watu hao kumsafirisha ambapo usiku huu wameamua kumtupa maeneo ya Mafinga jirani na msitu wa Sao Hill. Hata hivyo hakuwa na majeraha yoyote, japo inaelezwa alipotupwa alipoteza fahamu.
Abdul anadaiwa kuokotwa na kada wa CCM aitwaye Juma Dogan ambaye alimpa fedha ya taxi na kumuelekeza aende kituo cha Polisi Mafinga kuripoti kuhusu tukio hilo. Bwana Dogan ambaye ni mkazi wa Dar Es Salaam, anasema alikwenda Mafinga kwa shughuli za kibiashara, na ndipo alipokutana huko na tukio la Abdul na kuamua kumsaidia.
Abdul bado yupo kituo cha Polisi Mafinga na tayari ndugu zake wameshajulishwa.
Jana usiku majira ya saa 6, Abdul alituma ujumbe kwa rafiki yake akisema "Im at the high risk" akimaanisha yupo kwenye hatari kubwa, na baada ya hapo simu zake hazikupatikana tena hadi usiku huu alipookotwa huko Mafinga. Taarifa ya mawasiliano yake ya mwisho ilionesha kuwa simu yake ilituma ujumbe huo ikiwa maeneo ya barabara ya Sam Nujoma, Mwenge jijini Dar.
Bado haijafahamika waliomteka ni akina nani, na walifanya hivyo kwa lengo gani.
Abdul ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la wanafunzi wa elimu ya juu nchini, mwishoni mwa mwezi uliopita alifanya mkutano na waandishi wa habari kulaani mauaji ya mwanafunzi mwenzao Aquilina Aqueline aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi. Abdul na wenzie walitoa wito kwa Waziri Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Siro wajiuzulu au wafutwe kazi.!

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search