Wednesday, 21 March 2018

AMUUA MKEWE KISHA KUMZIKA KWENYE MTI WA MBUYU SINGIDA


Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina Bernard Shumba mkazi wa Singida anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa kumuua mke wake miaka minane iliyopita kisha kuuficha mwili wa marehemu kwenye mbuyu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Deborah Magiligimba, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa baada ya kukamatwa alikiri kutenda kosa hilo na kwenda kuonyesha mwili wa marehemu aliokuwa ameuhifadhi ndani ya mbuyu ambapo jeshi hilo kushirikiana na wananchi limefanikiwa kupata mabaki yake.


Inadaiwa kuwa mnamo Julai 10, 2010 katika Kijiji cha Yulansoni Kata na Tarafa ya Kinyangiri Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Tabu Robert (28) ambaye kwa kabila ni Mnyiramba, mkulima wa Yulansoni, aliuawa na mume wake aitwae Bernard Shumba Siza (47), Mnyiramba na mkulima wa Yulansoni.


Baada ya Mmuhumiwa kufanya tukio hilo aliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuficha kwenye mti wa mbuyu ambao una tundu kubwa na kisha aliripoti polisi kituo kidogo cha Kinampanda Mkalama kuwa mke wake ametoroka na alianza kumtafuta hadi tarehe Machi 17, 2018 ambapo taarifa zilipopatikana kuwa alimuua.


Baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kuhojiwa alikiri kufanya kitendo hicho na kuonyesha sehemu alipouficha mwili huo Machi 18, mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni.


Mkuu wa polisi kituo cha Mkalama na timu yake ya makachero walifika eneo la tukio na kufanikiwa kupata mabaki ya mifupa yakiwa ndani ya mti huo. Baadhi ya mifupa imechukuliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa mkemia wa serikali na iliyobakia ndugu wamekabidhiwa kwa ajili ya mazishi.


Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search