Tuesday, 13 March 2018

BARAZA LA WAZEE CHADEMA LATAKA KUONANA NA RAIS MAGUFULI

Baraza la Wazee wa Chadema limemuomba Rais John Magufuli kukutana na wazee ili kubadilishana nao mawazo sambamba na kumpa ushauri wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.


Akizungumza leo Jumanne Machi 13, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, katibu mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka amesema kumekuwa na mambo mengi yanayopigiwa kelele, ni vyema rais akakutana na wazee ili wamueleza mambo hayo.


“Ni lazima kama Taifa tuchukue hatua mapema kabla hatujachelewa. Rais Magufuli akubali kuitikia wito wa kukutana na wazee ambao watakuwa na ujasiri wa kumshauri ili kuepusha Taifa kuingia kwenye majanga,” amesema.


Amesema suala la wazee kukutana na rais, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu na kwamba nchini Kenya viongozi wameweza kukaa meza moja na kumaliza tofauti zao.


“Lazima tukae tujue mustakabali wa Taifa hatuwezi kusema hakuna tatizo. Tunamtaka akutane na wazee, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa tuzungumze kwa kuwa hii ni nchi yetu wote na si ya chama kimoja,” amesema.


Amesema mambo yanayopaswa kuzungumziwa ni suala la Katiba Mpya, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.


Amesema pia matukio ya watu kutekwa na kuuawa yameongezeka, “miezi sita iliyopita tulizungumzia mambo haya lakini naona ndio yanaongezeka.”“Wazee tumeumizwa mno kuhusu suala la Abdul Nondo hasa pale Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) alipotoa kauli kuwa kijana huyu alijiteka. Tulitegemea polisi wafanye uchunguzi, sasa kama waziri mhusika tayari ameshatoa hukumu tutegemee nini kwa hawa polisi. Tunajenga nini ndani ya mioyo ya hawa vijana ambao walijitoa kumtetea kijana mwenzao kama si chuki.”
Braza la wazee wa CHADEMA kupitia kwa katibu mkuu wake, Lodrick Rutembeka wamezungumzia kukamatwa, kubambikiziwa kesi, kuteswa, kutekwa, kushambuliwa hata kuuawa kwa viongozi wa kisiasi hata wananchi wengine wanaoonekana kukosoa utendaji wa kazi wa Rais Magufuli na serikali kwa kutumia rejea ya matukio kama la Tundu Lissu, kuuawa kwa kaimu mwenyekiti wa CUF jimbo la Matopetope, Ali Juma Suleyman.

Pia miili ya watu waliouawa iliyokuwa ikiokotwa kwenye fukwe ilhali serikali ikitoa taarifa tatanishi na taarifa zinazotoa majibu mepesi kwa maswali magumu. Ikiwemo kusema wanaookotwa ni wakimbizi.

Tatu ni kuminywa kwa haki za kikatiba na kisiasa kinyume na sheria za nchi, mfano kuzuiliwa kwa shughuli za kisiasa. Nne ni kuminywa kwa uhuru wa maoni na kupata taarifa ikiwemo kuzuiwa Bunge mubashara na kufungwa kwa magazeti.

Mihimili ya mahakama na bunge kuingiliwa na mhimili wa serikali.

Baraza la wazee CHADEMA limesema halitonyamaza kimya kwani yamkini serikali inaweza ikasikia, limetoa ushauri kwa Rais na serikali kuchukua hatua kwani ni vizuri kusikiliza kelele na kilio kwenye mitandao pamoja na mikutano ya hadhara kupigwa marufuku kwani na kutoa kauli tata zinaweza kuwapeleka mahakama ya ICC. BARAZA LIMESHAURI

  1. Rais Magufuli ambae ni mzee mwenzao aongoze kwa busara na kiongozi na hekima ya mtu mzima. Akubali kuitikia wito wa kukutana na wazee katika kikao kimoja ambao watakuwa na ujasiri wa kumwambia ukweli na kutoa ushauri wa kulipusha taifa kuelekea katika janga. Wamesema kukubali kuzungumza sio kukubali kushindwa na kutolea mvutano kati ya Marekani na Korea kaskazini pia nchini Kenya ambapo Rais wa Kenya amekutana na mpinzani mkuu kuzungumzia tofauti zao.
  2. Awe tayari kusikiliza na kupokea ushauri na ukosoaji kama alivyo tayari kupokea hongera pamoja na kupata sifa ya kuweza kuongoza malaika mbinguni.
  3. Kwa ajili ya kutibu majeraha na kuondoa makovu yanayosababishwa na mwenendo wa kisiasa nchini kwa sasa, suluhu la kudumu ambalo litaweka taifa pamoja ni katiba hivyo ni wakati muafaka kuzungumzia katiba mpya kuelekea uchaguzi wa 2020.


Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search