Wednesday, 28 March 2018

CAG aonya ukubwa wa deni la Taifa kwa GDP tushafika 73% ikifika 76% itakuwa shida, Magufuli asema wataendelea kukopa

[​IMG]


Kwa ufupi
Rais alitoa ufafanuzi huo baada ya awali, Profesa Assad kutahadharisha kwamba kiwango cha deni hilo kilichofikia cha Sh46trilioni kutoka Sh41trilioni kwa mwaka uliopita (2015/16)


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemtoa wasiwasi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuhusu Deni la Taifa, akisema nchi inakopa fedha na kuzitumia kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akipokea ripoti ya ukaguzi ya CAG mwaka 2016/17, Rais Magufuli alisema uwekezaji katika miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme wa Stieglers Gorge, utasaidia kukuza uwezo wa Serikali kulipa deni hilo.

Rais alitoa ufafanuzi huo baada ya awali, Profesa Assad kutahadharisha kwamba kiwango cha deni hilo kilichofikia cha Sh46trilioni kutoka Sh41trilioni kwa mwaka uliopita (2015/16) sawa na ongezeko la asilimia 12, kinatia wasiwasi na kwamba Serikali inatakiwa kuchukua hatua kupunguza ukubwa wa deni hilo.

“Tulichosema hapa kwa kweli ukuaji wa deni tunasema ni himilivu lakini jinsi linavyoongezeka, tunakaribia maeneo ya wasiwasi. Asilimia 72 ya GDP (Pato la Taifa) si mbaya lakini ikifika asilimia 76 ya nchi nyingine zimepata shida, inabidi tuangalie sasa namna gani tunaweza ku-control (kudhibiti) ukuaji wa deni hilo,” alisema Profesa Assad.

Katika ufafanuzi wake Rais Magufuli alisema miradi hiyo mikubwa imechagiza baadhi ya wahisani kujenga matumaini ya kuendelea kutoa ushirikiano na wameanza kurejea baada ya kuona Serikali ikiitekeleza kwa kutumia fedha za ndani.

Alisema Serikali inazo fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa na umeme.

Akitoa maoni yake kuhusu deni hilo, Profesa wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humphrey Moshi alisema wasiwasi wa deni hilo unaweza kuchagizwa na aina ya mkopo, akisema ipo ya riba nafuu ya marejesho ya muda mrefu.

“Tunaita non- concessional, lakini kuna mikopo ya riba kubwa,” alisema.

Alitaja mambo matatu ya kuzingatia katika kudhibiti ukuaji huo wa deni kuwa ni pamoja na kuangalia upya mikataba ya misamaha ya kodi kwa kampuni za kigeni nchini.

Alisema tafiti kadhaa zinaonyesha misamaha hiyo inatengeneza mazingira ya Taifa kuibiwa kodi.

“Pili, Serikali inatakiwa kuongeza kasi ya udhibiti ukwepaji kodi na kasi ya ukusanyaji kodi, lakini (tatu) Serikali inatakiwa kutekeleza miradi haraka inayotokana na mikopo ili kuepuka mazingira ya ufisadi.”


Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search