Tuesday, 27 March 2018

Freeman Mbowe na viongozi wa juu wa CHADEMA wafikishwa Mahakamani Kisutu-wasomewa mashataka nane


index.jpeg
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine 4 wa chama hicho wamefikishwa mahakama ya Kisutu, baada ya kuwekwa Mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi Dar. Waliofikishwa Mahakamani ni Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, Katibu Mkuu CHADEMA Dr. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara wa CHADEMA John Mnyika, Naibu katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake 5 wameingizwa katika ukumbi namba moja wa mahakama ya wazi Kisutu. Wanakabiliwa na mashtaka nane

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa chama hicho wamesomewa mashtaka manane katika Mahakama ya Kisutu ikiwemo kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa la kwanza ni kufanya mkusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali.

Kwa pamoja wanadaiwa Februari 16, 2018 wakiwa barabara ya Mkwajuni kwa pamoja walikusanyika kwa lengo la kutekeleza mkusanyiko ili watu waliokuwepo eneo hilo waogope kuona maandamano ya kuvunja amani.

Kosa la pili ni kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali, ambapo linawakabili washtakiwa wote wakidaiwa kutenda kosa hilo Februari 16,2018 Barabara ya Kawawa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni.

Kwa pamoja wanadaiwa wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani wakiwa katika maandamano na mkusanyiko wa vurugu waligoma kutii amri ya kusambaratika na kuvunja mkusanyiko huo uliosababisha kifo cha Akwilana Akwiline na majeraha kwa maofisa wa Polisi.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa jingine ni kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali, ambalo linamkabili Mbowe.

Inadaiwa Februari 16, 2018 akiwa viwanja vya Buibui Kinondoni DSM akihutubia wakazi wa maeneo hayo na DSM alitoa matamshi ambayo yangesababisha chuki kwa Jamii.

Pia kosa jingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi na kusababisha chuki katika jamii, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018.

Inadaiwa akiwa Uwanja wa Buibui Kinondoni DSM akihutubia wakazi wa DSM alitoa matamshi ambayo yangepelekea chuki katika Jamii.

Pia Mbowe anakabiliwa na kosa jingine la uchochezi wa uasi, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni DSM.

Inadaiwa akiwa na nia ya kupandikiza chuki na dharau dhidi ya uongozi uliopo madarakani alitoa maneno ambayo ni wazi yangesababisha uasi.

Pia kosa jingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi wa uasi, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui, Kinondoni DSM.

Inadaiwa akihutubia mkutano wa hadhara alitoa matamshi ambayo yangepandikiza chuki na dharau kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya uongozi uliopo madarakani.

Kosa la saba linamkabili Mbowe ambalo ni ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai, ambalo amelitenda Februari 16, 2018 maeneo ya Buibui Kinondoni DSM.

Inadaiwa Mbowe akiwa amejumuika na watu wengine aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutenda kosa.

Katika kosa la 8, Wakili Nchimbi amedai linamkabili Msigwa ambalo ni kushawishi raia kutenda kosa la jinai.

Msigwa anadaiwa ametenda kosa hilo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni DSM, ambapo aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana ambapo Wakili Nchimbi amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Hata hivyo, Wakili Nchimbi aliwasilisha maombi kwa mahakama hiyo ili washtakiwa wanyimwe dhamana kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania.

Kesi inaendelea.

UPDATES: 1845hrs

Viongozi sita wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wamenyimwa dhamana. Wamepelekwa Mahabusu hadi Alhamis tarehe 29 Machi, 2018 ambapo uamuzi wa kupewa dhamana au la, utatolewa. Wamepelekwa Gereza la Segerea.

Habari zaidi...

MWENYEKITI wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho ambao wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wamepelekwa mahabusu baada ya upande wa Jamhuri kuwasilishwa maombi ya kuwanyima dhamana.

Mbali ya Mbowe wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Bara Salum Salum, Mbunge wa Kibamba John Mnyika, Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiko na Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Vicent Mashinji.

Hivyo baada ya kusikiliza mabishano marefu ya upande wa Jamuhuri na ule wa utetezi juu ya dhamana ya washtakiwa kama wapate au la, mahakama imesema itatoa uamuzi Machi 29 mwak huu, mshtakiwa Mbowe na wenzake wamepelekwa rumande.

Mapema upande wa Jamuhuri uliwasilisha mahakamani hapo maombi ya kunyimwa dhamana kwa washtakiwa kwa njia ya mdomo.

Akiwasilisha sababu za kupinga dhamana mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Mkuu Dk.Zainabu Mango amedai ni kwasababu za usalama wa jamii na nchi kiujumla kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka.

Amedai wanatambua dhamana ni haki ya mshtakiwa lakini hakuna haki isiyokuwa na wajibu kwa mujibu wa katiba ya nchi. Kwani Mashtaka yao wanaashiria kutokutii amri yao kikatiba, utekelezaji wa haki binafsi unapaswa kuzingatia haki za watu wengine.

Alidai makosa yanayowakabili yanahatarisha usalama nchi na kuwapa dhamana ni kuendelea kuwapa nafasi ya kuendelea kufanya makosa hayo

"Jukumu la dhamana liko chini ya mahakama hii, hata hivyo kabla ya mahakama kutumia mamlaka yake kutoa ama kuzuia dhamana inapaswa kuangalia mazingira ya kosa husika"amedai Dk.mango.

Ameiomba Mahakama kuzingatia maslahi ya umma kwa ujumla wake kwa hatari ya makosa wanayoshtakiwa nayo na usalama wa taifa.

Wakili Faraja alidai kuwa kama washtakiwa wataruhusiwa kurudi uraiani baada ya matamko hayo ni wazi kwamba haki ya upande wa pili itapotea, matamshi yaliyotolewa na washtakiwa yana madhara endelevu kwa watanzania kwani tuna taarifa za upelelezi kwamba baadhi ya mambo yaliyoongelewa, ushawishi uliotolewa unaonekana kuna utekelezaji wa kihalifu.

Akijibu hoja hizo Wakili wa utetezi Peter Kibatala amedai hakuna chochote cha kisheria kilichozungumzwa kutoka kwenye dawati, Kilichoko mbele ya mahakama sio maombi ni pingamizi la dhamana na hakuna ushahidi wowote kwa yaliyosemwa.

Pia Kibatala amedai Wakili anashindwa kutofautisha askari mpelelezi na mawakili wasomi na Mahakama haiwezi kumnyima mtu dhamana kwa taarifa ambazo haziko mahakamani.

Aliendelea kudai hati ya mashtaka haina jina wala sahihi ya aliyeandaa jambo ambalo limekatazwa na Mahakama Kuu.

Chanzo: Michuzi

---------------
1.jpeg 2.jpeg 3.jpeg 4.jpeg 5.jpeg 6.jpeg

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search