Friday, 2 March 2018

Kailima: Nimeenda jandoni kwa hiyo siwezi kujibu matusi ya Mbowe

pic%2Bkailima.jpg 

Baada ya mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kuilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai ya kutotenda haki, mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo, Kailima Ramadhan amesema hawezi kujibu ‘matusi’ ya kiongozi huyo kwani ameenda jando.


Kwenye mkutano mwanzoni mwa wiki, Mbowe alilalamikia kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi kulikofanywa na NEC pamoja na taasisi nyingine za umma dhidi ya Chadema na akadai Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipendelewa.


Kwenye malalamiko yake, Mbowe alisema hajawahi kuona tume inayoingiliwa na Serikali kama hiyo ambayo alidai inaiba kura bila kutumia weledi tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Wizi unafanywa kwa mbinu za kitoto kabisa. Tumetuma barua kwa Kailima lakini hakujibu, hata tulipompigia hakupokea simu,” alilalamika mwenyekiti huyo.


Licha ya NEC, Mbowe pia aliilalamikia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa pamoja na Jeshi la Polisi, lakini juzi polisi na CCM walijibu na kumtaka Mbowe kuacha siasa za malumbano.
Akizungumzia malalamiko ya kiongozi huyo, Kailima alisema alikuwa safarini kikazi, lakini amemsikiliza Mbowe kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa hotuba yake na akasikitika sana.


“Nimesikitishwa sana na kiongozi wa ngazi za juu kutamka matusi hadharani. Mimi nimeenda jandoni siwezi kumjibu matusi hayo,” alisema Kailima.
Ukiachana na masikitiko hayo binafsi, Kailima alisema NEC inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni, maadili na miongozo ya uchaguzi na wakati wote wanapomjibu mtu huwa wanazingatia maeneo hayo.


Kuthibitisha hilo alimtaka Mbowe kujiuliza ni lini aliwahi kujibiwa kwa kunukuu vifungu vya sheria zisizokuwepo.
“Sasa tatizo ni sheria zilizopo au anayezitumia? Kama changamoto ni sheria, hilo si la tume. Sisi tunazitumia sheria zilizotungwa na Bunge,” alisema Kailima.


Aliitumia fursa hiyo pia kupinga hoja ya kutojibu barua za chama hicho kikuu cha upinzani nchini. Kailima alisema kumbukumbu zilizopo ofisini kwake, kati ya Februari 6 na 7 wakati kampeni zinaendelea Kinondoni, Chadema iliandika barua mbili zenye malalamiko tisa ingawa ziliwasilishwa Februari 12.


Malalamiko yaliyokuwamo ni kuhamishwa kwa vituo 46 bila kushirikishwa kwa Chadema. Mkurugenzi huyo alisema kwenye kikao cha Januari 31 kati ya tume na vyama vya siasa, Chadema iliyowakilishwa na Mustafa Muro na Shaaban Victor walikubali kuhamishwa kwa vituo hivyo kutokana na changamoto ya mazingira.
“Vipo (vituo) vilivyokuwa kwenye zahanati, kingine kwenye jengo la msikiti. Vyama vyote vilikubali kuhamishwa,” alisema.


Chadema pia walilalamikia wakuu wa wilaya kushiriki kampeni na walijibiwa kuwa kwa mujibu wa tume ya maadili, viongozi hao wamepotoka na wakashauriwa kupeleka malalamiko yao kamati ya maadili ya jimbo ambayo huwa na wawakilishi wa vyama vyote na iwapo wasingeridhika waende tume, lakini hawakufanya hivyo.


Pia, Chadema ililalamika kuadhibiwa na kamati ya maadili kutokana na kosa la mwanachama wake na tume ikawaambia wapeleke malalamiko yao kamati ya maadili ngazi ya tume ambayo huwa na wajumbe wa vyama vyote, lakini hawakufanya hivyo.


“Kwenye barua hizo, Chadema pia walilalamika kuwa kamati ya maadili inaendeshwa na makatibu tawala wa wilaya (ma-DAS),…hili si kweli. Ma-DAS si wajumbe, na kamati hii haiendeshwi nao,” alisema Kailima na kuongeza:
“Tukawaambia, hili ni kosa la maadili hivyo waende kamati ya maadili na wasiporidhika waje tume na wakiona hawajatendewa haki mpaka huku kwetu basi waende mahakamani kulalamika kuwa hawakutendewa haki pia.”


Licha ya barua hizo, Kailima alisema Februari 15, Chadema waliwasilisha barua nyingine mbili; moja mchana na nyingine saa moja usiku na kufafanua kuwa kipindi cha uchaguzi huwa wanafanya kazi mpaka usiku.
Kwenye barua hizo, alisema kulikuwa na hoja tano. Miongoni mwa hoja, anasema Chadema walilalamika msimamizi wa uchaguzi kukataa kuwaapisha mawakala wao 15 wa ziada.


“Mimi nikauliza kwenye hiyo barua, hao mawakala mbadala watawekwa wapi kwani kanuni zinataka wakala mmoja kuwepo kwenye kituo kimoja,” alihoji.
Chadema pia walilalamika msimamizi wa uchaguzi Kinondoni kukataa kuwapa mawakala wao barua na fomu za viapo, suala walilolifanya kabla ya muda ambao msimamizi huyo alikubaliana na mawakala wa vyama vyote.


Akihitimisha hoja zake, Kailima alisema: “Kupendwa au kutopendwa kwa majibu ya tume si suala letu. Sisi tunatumia sheria zilizopo, asiyependa aangalie mapungufu yaliyopo kwenye sheria zilizopo.”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search