Tuesday, 6 March 2018

MASHEIKH WALIOPOTEA ZANZIBAR WAPATIKANA

Masheikh watano waliotekwa na watu wasiojulikana katika mazingira ya kutatanisha visiwani Zanzibar, hatimaye wamepatikana.

Kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Amir Haji Khamis Haji na wenzake wanne waliotoweka Februari 9, mwaka huu, waliachiwa juzi na kuungana na familia zao.

Akizungumza baada ya kuachiwa na watu hao, Amir Haji, alisema baada ya kukamatwa na watu hao, alifungwa kitambaa usoni na kupelekwa asikokujua na watu hao wasiojulikana.

“Binafsi siwajui hata waliofanya hivyo, lakini hadi leo hii (juzi) kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu milango ya asubuhi saa tano na nusu, naona nimeachiwa huru bila kuwa na madhara yoyote ikiwemo kuuawa.

“Na sasa niko nyumbani ni mzima, sikupata athari ya kupigwa na kitu chochote, kwahiyo nawaomba Waislamu wote waridhike na hilo, tuwe pamoja na waniombee dua mzee wao, hakuna kilichoharibika.

“Tuendelee na tuko pamoja na tuhifadhi mambo ya baadaye Inshallah. Sikuulizwa maswali yoyote, naona wao walikuwa wakifanya kazi yao, nasi kwa upande wa dini tunafanya pia.

“Kitu muhimu ni kuangalia masilahi ya baadaye na kuweka amani na hawa waliofanya haya nafikiri walikuwa wakifanya haya kwa ajili ya kuweka amani,” alisema Amir Haji.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search