Monday, 5 March 2018

Msajili akataa maelezo ya CHADEMA kuhusu kukiuka sheria ya vyama vya siasa na kanuni za maadili ya vyama

MSAJILI+PIC.jpg 
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameeleza kutoridhishwa na maelezo yaliyowasilishwa na CHADEMA kuhusu tuhuma zinazowakabili za kukiuka sheria ya vyama vya siasa na kanuni za maadili ya vyama hivyo.

Mbali na kueleza hayo, msajili ametoa siku tano nyingine kwa CHADEMA kujieleza kwa nini chama hicho kisichukuliwe hatua kwa kukiuka sheria na kanuni hizo.

Barua ya Jaji Mutungi ya Machi Mosi kwenda kwa katibu mkuu wa CHADEMA ambayo Mwananchi imeiona imetoa siku tano kuanzia Machi 2 hadi 6, chama hicho kiwe kimewasilisha maelezo mengine.

Jaji Mutungi ameandika barua hiyo baada ya kutoridhishwa na maelezo yaliyowasilishwa na CHADEMA aliyoiandikia barua ya awali akiipa siku tano kuanzia Februari 21 hadi Februari 25.

Msingi wa barua za Jaji Mutungi unatokana na tuhuma kwa CHADEMA kufanya maandamano Februari 16 kutoka Mwananyamala kwenda ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala wa uchaguzi mdogo uliofanyika Februari 17.

Katika maandamano hayo kuliibuka vurugu kati ya polisi na waandamanaji katika eneo la Kinondoni Mkwajuni.

Wakati wa vurugu hizo, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini (22) aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji.

CHADEMA katika majibu ya barua ya awali ya Jaji Mutungi ambayo amesema hajaridhishwa nayo ilitoa hoja kadhaa huku ikihoji hatua alizochukua mpaka sasa kufuatia mfululizo wa matukio ya mauaji ya viongozi wake.

Kaimu katibu mkuu wa CHADEMA, John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari Februari 23 kabla ya kupeleka majibu ofisi ya msajili alisema Jaji Mutungi hakuwaeleza mlalamikaji wa tuhuma zinazowakabili.

“Tunaelewa kwamba msajili anasukumwa na Serikali. Dhamira yao ni kuifuta CHADEMA . Nawaambia jambo hilo hawaliwezi,” alisema Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba.

Jaji Mutungi katika barua ya Machi Mosi ambayo pia Mwananchi imeiona anasema, “nimesoma vyema barua yako, ila nasikitika kwamba barua yako haikujielekeza kujibu hoja ya msingi ambayo ilihitaji chama chako kitoe maelezo kuhusu uvunjifu wa kanuni za maadili ya vyama vya siasa na sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992, hususan kauli ya mwenyekiti wa chama chenu, Freeman Mbowe ambaye katika mkutano wa kufunga kampeni za chama chenu uliofanyika Mwananyamala kwa Kopa, Februari 16 alisikika akiongea maneno ya uchochezi.”

Ananukuu kauli ya Mbowe akisema, “Nitaongoza mapambano nchi hii, nitaongoza mapambano nchi hii, lazima tukubali kubeba majeneza lazima tukubali kubeba nini? Matokeo ya Watanzania 100 watakaokufa wataleta haki katika nchi hii.”

Jaji Mutungi anasema katika barua hiyo, “Hivyo, narudia wito wangu kukitaka chama chako kuwasilisha maelezo ndani ya siku tano kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa na kanuni za maadili ya vyama vya siasa.”

Alipotafutwa Jaji Mutungi jana kuelezea barua ya majibu ya CHADEMA na uamuzi wa kuwaandikia barua nyingine hakupatikana, huku msajili msaidizi, Sisty Nyahoza akieleza yupo shule akiendelea na mitihani hivyo asingeweza kulizungumzia suala hilo.

Akizungumzia barua hiyo, mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA , John Mrema alisema, “tutamjibu kesho (leo) Jumatatu. Ila tunamshangaa msajili anajipa mamlaka ya kuwa mdhibiti kinyume kabisa cha sheria ya vyama vya siasa. Huyu ni jaji tulitarajia awe na weledi wa kuitafsiri sheria ambayo anaisimamia na si kama anavyofanya sasa nje ya sheria.”


Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search