Wednesday, 21 March 2018

NONDO KUMPANDISHA IGP SIRRO KIZIMBANI

Mahakama Kuu nchini imetoa wito wa kuwaita DCI, IGP na AG kufika mahakamani siku ya Jumatano ya tarehe 21 kujibu kesi ya kutomfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP) Abdul Nondo.

Taarifa za wito huo umetolewa na Wakili wa Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Wakili Jebra Kambole ambaye ametoa taarifa hiyo fupi kupitia kwenye ukurasa wake maalum wa Twitter.

Kambole amesema "Wito umetolewa leo Mahakama kuu mbele ya Jaji Samejikwamba DCI, IGP na AG wanapaswa kufika mahakamani 21/03/2018 kujibu kesi ya Abdul Nondo".

Akizungumza na www.eatv.tv Kambole amesema washitakiwa katika kesi hiyo itakayosikilizwa Jumatano, Sirro ameitwa kwa sababu yeye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini hivyo vituo vyote na polisi wapo chini yake lakini bado Nondo amekuwa hapatikani katika vituo vya polisi.

Aidha Kambole amesema kuwa katika jalada lililofunguliwa leo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), naye kahusishwa kwa sababu mara ya mwisho Nondo alipokelewa na yeye alipofikishwa Dar es salaam kutoka Iringa na kwamba alimchukua kama muathirika wa tukio la utekwaji na siyo mshtakiwa.

Hata hivyo Kambole amesema ameshafanya jitihada nyingi za kutaka kuonana na mteja wake lakini hadi sasa juhudi zake hazijafua dafu.

Abdul Nondo anashikiliwa na jeshi la polisi tangu Machi 7,2018 ambapo awali aliripotiwa kupotea kusikojulikana na kesho yake kujikuta Iringa ambapo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa amesema mpaka sasa wanamshikilia Nondo kwa ajili ya upelelezi na watakapokamilisha watamfikisha mahakamani.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search