Tuesday, 13 March 2018

POLISI : NONDO ALIJITEKA,ALIKWENDA IRINGA KWA MPENZI WAKE....ATAFIKISHWA MAHAKAMANI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea kumshikilia Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kujiteka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 13, 2018 Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.

Alisema uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi kuhusu taarifa za kutekwa kwa Abdul Nondo umetoa na kuwa mwanafunzi huyo alijiteka mwenyewe.

Mambosasa alisema Nondo alikamatwa huko Mafinga Iringa akiendelea na shughuli zake na kusema hakuripoti sehemu yoyote kuhusu kutekwa kwake na kudai kuwa wamebaini kijana huyo alikwenda kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara. 

"Pengine alitaka kuzua hilo ili kujipatia umaarufu ila upelelezi uliendelea kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa hii ni baada ya kufanya uchunguzi wa kisayansi na kubaini muda ule aliosema ametekwa simu yake imeendelea kuonyesha mawasiliano aliyokuwa anafanya na huyo binti ambaye alikuwa amemfuata" ,alieleza.

Mambosasa amesema kuwa walipomkamata walikuwa na mashaka kuwa huenda akawa amepatwa na ugonjwa wa malaria ya kichwa iliyopelekea kufanya hayo na kudai kuwa alipelekwa hospitali na kupimwa na kuonekana kuwa mzima asiye na matatizo yoyote ya kiakili. 

"Alikuwa ni mzima wa afya njema na haya aliyafanya kwa makusudi kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, jeshi la polisi limebaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa huru baada ya kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alisafiri akiwa huru na akafika Iringa akiwa salama, kwa hiyo ni uzushi mtupu uliokuwa na malengo ya hovyo lakini kuna watu wengine walilishabikia jambo hili wengine huwezi kuamini kwa nafasi zao walilishabikia jambo hili la hovyo mtu kujizushia jambo"alisema Mambosasa 

Nondo alidaiwa kutoweka Machi 6, 2018 lakini alijisalimisha mikononi mwa polisi wilayani Mafinga, Iringa Machi 7.

Baada ya kujisalimisha alifunguliwa jalada la uchunguzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire ambaye aliwaeleza wanahabari kuwa uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo ni kweli alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani.

Machi 10, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa litakapomalizana na Nondo limrejeshe jijini Dar es Salaam ili na yeye aanzishe uchunguzi wake kwa mwanafunzi huyo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search