Wednesday, 21 March 2018

RAIS ALALAMA PESA ZA MRADI WA KUNUNUA WAPINZANI KULIWA NA WAJANJA

 
Rais wa Zambia Edgar Lungu ameshtushwa kusikia wanachama wa chama kikuu cha upinzani cha UPND wanaonunuliwa kujiunga chama tawala cha PF wanalipwa K20,000 na wengine K5000 badala ya kiasi kilichotengwa cha kati ya K200,000 na K500,000.
Haijajulikana chanzo cha fedha hizo kama ni chama au serikali lakini kiasi kikubwa cha fedha kimeidhinishwa na rais kwa ajili ya mradi wa kununua madiwani wa chama cha United Party for National Development (UPND) kinachoongozwa na Hakainde Hichilema.

Lungu alionyesha mshtuko huo alipozungumza na maofisa waandamizi wa chama tawala cha Patriotic Front (PF) kwenye Ikulu muda mfupi baada ya kurejea nchini akitokea Afrika Kusini kwa shughuli binafsi.

Rais alimwambia Davies Mwila kwamba kila diwani anayehama kutoka UPND alitakiwa kulipwa kiasi kinachofikia K200,000 wakati wale kutoka kwenye ngome za UPND kama vile jimbo la Kaskazini Magharibi walipaswa kupewa hadi K500,000.

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya madiwani wa UPND walikiri kuwa wanalengwa kushawishiwa kuhamia PF baada ya kupewa K20,000 wakati wengine walipewa kiasi kidogo cha K5000.

Pia madiwani hao walidanganywa kwamba wakihamia PF watateuliwa kuwa wakuu wa wilaya au kupewa kazi nyingine serikalini lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichofanyika.

“Waungwana, imekuwaje tunajikuta katika aibu ambapo sasa madiwani UPND wanabadili mawazo yao? Kaizar Zulu alikuja hapa akaniambia tutekeleze mpango wa kisiasa wa kupata madiwani wa UPND kote nchini," alisema.

“Bajeti niliyoletewa na kuiidhinisha na fedha zikatolewa ni kwamba kila diwani wa UPND ambaye anakubali kujiuzulu katika maeneo kama Kaskazini, Luapula, Copperbelt, Mashariki na Muchinga walitakiwa kupewa K200,000 pamoja na kazi ya maana. Wale wa majimbo ya Kaskazini Magharibi, Magharibi na Kusini walitengezwa K500,000 kila mmoja pamoja na gari na kazi kwa kuwa tusingeweza kutetea viti vyetu kule. Tulitaka tu kupima umaarufu wetu katika maeneo yale.

“Lakini ni dhahiri fedha zilizotolewa hazikuwafikia madiwani waliolengwa. Sasa ni nini kinachoendelea?" alihoji Lungu wakati akiomba kupewa ripoti kamili."

Maoni ya PF
Lakini vyanzo kutoka ndani ya PF vimesema kuna watu kama Kaizar Zulu wanaodhoofisha uongozi wa Edgar Lungu.

Walifichua kwamba Lungu anadanganywa kwamba ana umaarufu wa kiwango cha juu na yeye anaendelea kutoa fedha ambazo zinaingia kwenye mifuko ya wale wanaomwona kuwa hawezi kufika popote.

"Kinachotokea ni kwamba ni wazi kabisa kuwa watu wengine wananufaika na hali hiyo na ukosefu wake wa ujuzi wa siasa sahihi nchini. Wanamwambia kwamba bado anajulikana sana na atashinda tena kwa kishindo. Jambo la kushangaza ni kwamba yeye pia anakiamini kikundi hiki kidogo kinachomzunguka. Lakini kile ambacho hajui ni kwamba hili ni kundi la wahuni ambao wanajali biashara zao," kilisema chanzo kutoka PF.

"Kazi yao ni kupora tu rasilimali za umma hata kutoka kwake na kununua mali zao. Je, unaweza kufikiri kwamba Rais wetu hakuwa anajua hata kiwango ambacho Rais wa UPND Hakainde Hichilema ameingia maeneo kama vile majimbo ya Mashariki na Kaskazini.”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search