Wednesday, 21 March 2018

Ushiriki wa sekta binafsi katika Tanzania ya viwanda, Mengi akosoa ukadiriaji kodi kandamizi wa TRAAmeanza kuongea Dr. Reginald Mengi ambae anataja mambo 13 kutoka kwenye taasisi anayoiongoza na anaishukuru serikali kwa mamb kadhaa ikiwemo kushuka kwa riba na kuongezeka kwa mikopo kwenye sekta binafsi kwa asilimia 3.3 ikiwa ni matunda ya juhudi za serikali.

Pia amepongeza kuimarika kwa hali ya uchumi ikiwa ni kiwango cha juu kwa nchi zote za Afrika Mashariki. Amepongeza kwa kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ikiwa ni juhudi za Rais kuhimiza makusanyo ya kodi.

Mengi amekosoa ukadiriaji mbovu wa kodi kandamizi ambao imesababisha nyingi kufungwa. Dr. Mengi amesema mwezi Mei ndio utakuwa mwisho wa kuwa mwenyekiti wa TPSF kwani katiba inaruhusu mwisho mihula miwili na anawaomba radhi aliowakosea.

(Sauti ya ndugu Mengi leo haiko sawa na inasikika ikiwa na mtetemo na kushindwa kusoma kwa ufasaha).

Kwa sasa Rais Magufuli anaongoza kikao cha kusikiliza kero za wafanyabiashara ambapo kila mmoja amempa dakika tatu.

Wafanyabiashara wanafunguka na wameongelea kibali cha sukari, kodi ya makampuni ambayo Tanzania iko juu kuliko nchi za Uganda na Kenya, TRA kutorejesha kodi iliyozidi.

Anaeongea sasa ni Dr. Kimei anasema mabenki yanalazimika kushusha riba kwa sababu ya kushuka kwa riba ya benki kuu pia ameomba BRELA kuharakisha kuingiza taarifa za wateja.

Rais Magufuli: Kwanini sisi Tanzania hatuna kiwanda cha kuzalisha Industrial Sugar, kweli tumeshindwa? Suala la sukari limewagharimu watu wengi ikiwemo mawaziri toka enzi za Mkapa. Tulitaka tufanye uchambuzi wa kutosha, wapo waliokuwa wanaleta na kuifungasha upya na kuipeleka katika matumizi ya binadamu.

Rais Magufuli amesema ni viwanda nane pekee ambavyo viliagiza sukari ya kiwandani na kutumia kihalali bila udanganyifu ikiwemo SBC(Pepsi) na Bakhresa.

Pia Rais Magufuli ameelezea kuhusu serikali kufanya biashara na pesa zake na kusema serikali kutoa pesa zake benki na kutokwenda kukopa imefanya benki kuwakopesha watu wa kawaida na wafanyabiashara.

Rais Magufuli amesema ndani ya serikali na wabunge hawaoni tatizo la mafuta kuagizwa kwa sababu wakati wa Bunge, wafanyabiashara wanahamia Dodoma kufanya 'Lobbying' na bia kunywewa. Ametaka wanaoagiza wapigwe kodi kubwa hata mara mbili ili kuwa-discourage na wakamshtaki popote.

Amesema Tanzania hata ikikosa mafuta zitapondwa hata karanga au mafuta ya samli. Amesisitiza Tanzania inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya ajabu na mengine yamesha-expire.

Rais Magufuli amesema bajeti ya afya imepanda kutoka Bilioni 31 hadi 269 na Tanzania imepewa tenda ya ku-supply madawa katika SADC. Anasema hata Drip ya maji zimeagizwa Uganda kwa kutumia dola zaidi ya milioni 10.

=====

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki moja kuanzia tarehe 19 Machi, 2018 kwa Mawaziri kufanyia kazi na changamoto na maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara uliofanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo ametoa maagizo hayo wakati akihitimisha mkutano huo ambao wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali wamepata nafasi ya kueleza maendeleo ya shughuli zao, changamoto zinazowakabili na mapendekezo ya kuimarisha biashara na uwekezaji hapa nchini.

Miongoni mwa changamoto hizo ni utozaji wa kodi unaoathiri biashara na uwekezaji, urasimu wa taasisi za Serikali, udhibiti wa bidhaa za kutoka nje ya nchi zinazoathiri uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwepo wa sheria na kanuni kandamizi kwa biashara na uwekezaji na utendaji usioridhisha kwa baadhi ya maafisa wa Serikali.

Mhe. Rais Magufuli amewataka Mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ndani ya kipindi cha wiki moja ili Serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wafanyabiashara hao kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika uchumi wa nchi na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji hususani katika ujenzi wa viwanda.

“Nataka kuwaambia kwa dhati kabisa, Serikali ninayoiongoza haiwachukii wafanyabiashara, inawapenda na itawaunga mkono, kama nilivyowaambia huko nyuma huu ndio wakati wenu wa kufanya biashara, fanyeni biashara zenu na lipeni kodi, hizi changamoto tumezipokea na tutazifanyia kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa anayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga - Tanzania, na amewataka wafanyabiashara wanaofanya vitendo vya udanganyifu katika kodi na uingizaji wa bidhaa wabadilike.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kutaka utozaji wa kodi uangaliwe ili usiathiri shughuli za uwekezaji na uzalishaji, na amewataka wafanyabiashara kuendelea kufanya shughuli zao kwa amani kwa kuwa Serikali itaendelea kuwalinda.

Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Dkt. Reginald Mengi amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuimarisha uwekezaji zikiwemo kuimarishwa kwa sekta ya fedha, usimamizi mzuri wa uchumi na kuongezeka kwa mikopo.

Dkt. Mengi ametoa mapendekezo ya sekta binafsi yakiwemo kuiwezesha zaidi sekta binafsi ili iongeze uzalishaji na ulipaji wa kodi, kuweka vivutio vya kodi katika viwanda, kuimarisha miundombinu na vivutio vya kilimo, kupunguza urasimu katika uwekezaji, kuwepo mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa kodi na kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

19 Machi, 2018

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search