Tuesday, 24 April 2018

Ado Shaibu: Zanzibar Kisingizio tu kwenye kashfa ya TZS 1.5T

Image result for ado shaibu

-Hoja 5 za Ufafanuzi wa ACT Wazalendo Dhidi ya Uongo wa Makusanyo ya TZS Bilioni 203.9 kwa niaba ya Zanzibar ( Transfer to Zanzibar ).


Imetolewa na Ado Shaibu 

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi kwa niaba ya ACT Wazalendo 

24/4/2018


Aprili 20, Serikali ilitoa kauli bungeni, kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, juu ya shilingi 1.5 trilioni, zisizojulikana matumizi yake kwa mujibu wa ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2016/17. Katika majibu hayo, kuna hoja ya shilingi 203.9 bilioni, ambazo Serikali ya Muungano (SMT) imedai ni mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). 


ACT Wazalendo tumepitia nyaraka za ukaguzi, kimahesabu na za kibajeti za Serikali zote mbili, SMT na SMZ, ili kujiridhisha na taarifa hizo. Baada ya uchambuzi wa nyaraka hizo tumegundua kuwa Serikali kwa makusudi imeendeleza upotoshaji bungeni juu ya zilipo shilingi 1.5 trilioni. Tumelifafanua hilo kwa hoja tano (5) zifuatazo:


1. Bajeti ya Zanzibar na Vyanzo Vyake


Bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2016/17 ilikuwa ni shilingi 841.5 bilioni, shilingi 482.4 bilioni kutoka katika vyanzo vya ndani, shilingi 324.8 bilioni mapato ya nje (ruzuku - 93.3b, na mikopo - 231.5b), pamoja na 34.3 bilioni mkopo wa ndani.


Mchanganuo wa Makusanyo ya fedha za ndani ni kama ifuatavyo; Bodi ya Mapato Zanzibar, ZRB (237.4b), TRA Zanzibar (188.8), Mapato ya Mawizara (26.4b), Kodi ya Mapato ya Wafanyakazi (PAYE ) kwa watumishi SMT (21b), Gawio la faida kutoka BOT (4b), na Gawio la faida kutoka mashirika ya SMZ (4.8b). Maelezo haya yako kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya Zanzibar, 2016/17 iliyotolewa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) wakati akiwasilisha bajeti husika.


2. Makusanyo na Matumizi ya SMZ Mpaka Machi, 2017 


Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya SMZ kwa mwaka wa Fedha wa 2016/17 (iko kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya SMZ ya mwaka 2017/18 ) inaonyesha makusanyo ya SMZ mpaka Machi, 2017 yalikuwa ni shilingi 406.9 bilioni, kutoka vyanzo vifuatavyo; Ndani (389.6 bilioni) na Nje (58.6 bilioni). Katika vyanzo vya ndani, Mapato ya Kodi yalikuwa ni shilingi 366.0 bilioni (makusanyo ya ZRB na TRA), na Mapato yasiyo ya Kodi (23.6 bilioni)


Taarifa hiyo inaonyesha pia kuwa jumla ya Matumizi halisi ya SMZ mpaka Machi, 2017 yalikuwa ni shilingi 424.8 bilioni, shilingi 378.3 zikitokana na mapato ya ndani, na shilingi 46.5 zikitokana na ruzuku, mikopo na michango ya Washirika wa Maendeleo.


3. Makusanyo ya TRA ya Zanzibar Hubaki kwa SMZ, Hayatokei Kwenye Hesabu za SMT


Kikawaida makusanyo ya TRA Zanzibar hubaki Zanzibar, hutuzwa kwenye akaunti za SMZ Katika Benki Kuu na huhesabika kuwa ni mapato ya Zanzibar, Kamwe fedha hizi hazichanganywi na mapato ya Serikali ya Muungano. Makusanyo haya, pamoja na matumizi yake, hukaguliwa na Ofisi ya CAG Zanzibar. Hivyo basi, hesabu zake hazitarajiwi kutokea kwenye ripoti ya CAG iliyokabidhiwa bungeni.


Ndio maana taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2016/17 imeeleza namna makusanyo husika ya TRA na ZRB yalivyofanyika na namna fedha hizo zilivyotumika katika miezi 9 ya mwaka wa fedha 2016/17. Fedha zote za TRA Zanzibar kwa miezi hiyo 9 zimekusanywa na kubaki chini ya SMZ, na kutumika na SMZ bila kupitia SMT. 


Mpaka Machi, 2017, Fedha ambazo SMZ hawakuwa wamekusanya kutoka TRA Zanzibar ni mapato tarajiwa ya robo ya mwisho wa mwaka (Aprili - Juni, 2017) yaliyokadiriwa kufikia shilingi 52.8 bilioni tu. 


4. PAYE za Watumishi wa SMT Walioko Zanzibar Hukusanywa na SMT kwa Niaba ya SMZ 


Fedha pekee za mapato ya kikodi ambazo Serikali ya Muungano huzikusanya kwa niaba ya SMZ, ni fedha za makato ya Kodi (PAYE) za watumishi wa Serikali ya Muungano wanaofanyakazi Zanzibar, watumishi hawa ni kama Polisi, Wanajeshi nk. Fedha hizi hukusanywa kila mwezi na TRA makao makuu, hutunzwa kwenye akaunti ya hazina Benki Kuu ya Tanzania, na kisha hupelekwa hazina ya Zanzibar. 


Fedha hizi hukusanywa kila mwezi, na zinapaswa kupelekwa Zanzibar kila mwezi ili kugharamia shughuli mbalimbali za SMZ. Kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, matarajio ya makusanyo PAYE yalikuwa ni shilingi 21 bilioni. Kwa kuwa idadi ya watumishi hawa inafahamika, Wizara ya Fedha ya Zanzibar, wakati ikielezea utekelezaji wa Bajeti ya 2016/17, ilionyesha kuwa yalikusanywa yote kwa 100%.


5. Juni 30, 2017 akaunti ya Zanzibar BoT Ilikuwa na Shilingi Bilioni 14 tu. 


Fedha za Zanzibar kwenye akaunti zake Benki Kuu (BOT) zinaweza kuonekana kwa urahisi kwenye Hesabu za Benki Kuu. Hesabu za BOT kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2017 hazionyeshi uwepo hizo shilingi 203.9 bilioni ambazo SMT wanadai kuikusanyia SMZ. Hata wakati wa kufunga hesabu za BOT kwa mwaka 2016/17 fedha pekee zilizokuwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa ni shilingi Bilioni 14. Hivyo sio sahihi hata kidogo kwa Taarifa ya Naibu Waziri Fedha kuonyesha kuwa kulikuwa na ‘transfer to Zanzibar’ kutoka Makusanyo ya Mapato ya Serikali ya Muungano. 


Serikali Ijibu Maswali Haya. Isituhadae! 


Maelezo ya SMT bungeni ni kinyume na nyaraka za BOT, pamoja na taarifa za Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar. Ni vema sasa SMT ijibu chanzo cha mapato haya ya kikodi (203.9b) ni kipi? Kama fedha zilizokusanywa na TRA Zanzibar, zimeonywesha na SMZ kwenye BLW kuwa zimekusanywa, kubaki na kutumika Zanzibar, hizi SMT inazodai kuikusanyia Zanzibar na kukaa nazo kwa mwaka mzima ni zipi? Na ziko wapi? Fedha hizi zimekusanywa na kulipwa Zanzibar kupitia akaunti gani? Zanzibar wamepewa lini fedha hizi? Matumizi yake ni yapi kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa na BLZ? Je utaratibu wa makusanyo ya Zanzibar umebadilika na sasa Fedha za Zanzibar zinakaa Hazina ya Muungano? Kama utaratibu umebadilika, ulibadilika lini na je utaratibu mpya una ridhaa ya Baraza la Wawakilishi? 


Kwa taarifa ile ya Serikali Bungeni, mpaka Juni 30, 2017, ni wazi kuwa SMT bado ilikuwa imezishikilia fedha za SMZ, ambazo kikawaida hutolewa kila mwezi ili kuwezesha Zanzibar kujiendesha. Tukiamini kuwa huu ndio ukweli, na kuwa bunge halijadanganywa, basi ni dhahiri kuwa tunapaswa kuamini kuwa Serikali ya Zanzibar ilikuwa inajiendesha kwa MIUJIZA, ikikusanya mapato HEWA na kufanya matumizi ya KUFIKIRIKA ya mishahara, ruzuku, pensheni kwa wazee na miradi ya maendeleo.


Maana ni jambo lisiloweza kuingia akilini kuwa Fedha zote zinazokusanywa kwa niaba ya Zanzibar Katika mwaka 2016/17 hazikutolewa kwenda Zanzibar na kubakia Bara mpaka baada ya mwaka kuisha. Pia taarifa za mwenendo wa Akaunti za SMZ zilizoko BOT ni uthibitisho wa dhahiri kuwa hakukuwa na fedha za SMZ, shilingi 203.9 bilioni zilizoshikiliwa na SMT wakati au mara baada ya mwaka wa fedha wa 2016/17 kuisha. 


Kama SMT wanadai kubaki na fedha hizi kwa mwaka mzima wa fedha (2016/17), na kushindwa kuziwasilisha hesabu zake kwa CAG miezi mitatu baada ya mwaka wa fedha kufungwa (Septemba 2017), na hata kwenye Exit Meeting (Januari 2018), ni vema waonyeshe tu hata walikozitunza katika akaunti zao BOT.


Shilingi 1.5 trilioni ni karibu mara 2 ya bajeti yote ya Zanzibar, kupotea namna hii na maelezo ya kupotea kwake yawe ni uongo wa kuisingizia Zanzibar ni dharau kubwa kwa Zanzibar, ni kuidogosha Zanzibar, ni kitengeneza kero mpya ya muungano wetu kwa SMT kuitupia madudu yake SMZ, ni hadaa kwa umma, ni kutudharau Watanzania. Hatutakubali. Tutaendelea kuhoji ziliko shilingi 1.5 trilioni zetu mpaka tujue ziliko.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search