Monday, 30 April 2018

KAULI YA HECHE BAADA YA MDOGO WAKE KUCHOMWA KISU

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amefunguka kuwa mpaka sasa haelewi ni kwa vipi mtu anaweza kuuawa na polisi kwa kuchomwa kisu tena akiwa amefungwa pingu huku akikumbushia tukio la mdogo wake mwingine kujeruhiwa vibaya na polisi ambapo alisababishiwa ulemavu mwaka jana.

Mbunge Heche amesema kwamba mtu kuchomwa kisu mgongoni ni kudhamiria kuua kwasababu mtu huyo hakuwa anapambana. 

"Nilijua mikononi mwa polisi ni sehemu salama, wiki mbili zilizopita kijana Allen alikufa katika mazingira tata kule Mbeya, Mwanza mama aliyekamatwa na kunyimwa dhamana mtoto wake mchanga alikufa. Leo ni kwangu mdogo wangu ameuwawa kikatili sana mikononi mwa polisi. Maisha yangu yote nimeyatoa kupigania haki ili watu wasionewe, mtuhumiwa asifanywe mkosaji na kuhukumiwa kabla ya vyombo vya sheria kumhukumu," Heche.

Ameongeza " Mwaka jana mdogo wangu mwingine aliumizwa vibaya sana na polisi. IGP Mangu na RPC waliokuwa Tarime walilipa uzito suala hilo lakini walipoondolewa, suala liligeuzwa kisiasa na wale vijana waliokua wamemjeruhi mdogo wangu ambaye mpaka sasa sikio moja halisikii,wakarudishwa kazini kinyemera na kuhamishwa Tarime kama kunikomoa. Mimi nimewahi kutishiwa kuuwawa kituo cha polisi, najisikia maumivu makubwa mno lazima Watanzania wakatae hali hii".

Pamoja na hayo Mbunge huyo amehoji juu ya ukimya wa Waziri na kuongeza kwamba ni watu wangapi wanakufa na kuumizwa mikononi mwa polisi bila matukio kujulikana wala kutangazwa na kuweka wazi kwamba atazungumza muda ukifika.

WAKATI HUO HUO RPC ATHIBITISHA MDOGO WAKE HECHE KUUAWA NA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya Henry Mwaibambe amethibitisha kuuawa kwa Bwana Chacha Heche Suguta ambaye ni mdogo wa Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche, kwa kuchomwa kisu na Polisi.

Kamanda Mwaibambe amesema marehemu alikuwa na mgogoro na mmoja ya askari waliokuwa wamemkamata, na kufikia hatua ya kutaka kushikana (kupigana) ndipo askari aliposhindwa kujizuia na kumchoma kisu.

“Tukio ni la kweli limetokea na huyo askari tunamshikilia, huyo kijana alikamatwa usiku sasa wakati wapo kwenye gari wakielekea kituo cha polisi, ukatokea mzozo kati ya huyu askari na huyu marehemu, mzozo kama wanataka kupigana, mwenzake akaingilia kuamua, lakini ni kweli askari amemjeruhi huyu mgongoni, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi leo saa 6 mbele ya ndugu zake, kweli umekutwa na jeraha la hicho kisu mgongoni na mtuhumiwa alikuwa hajavalishwa pingu, ila hatujui nini waliambiana mpaka kufikia hivyo”, amesema Kamanda Mwaibambe.

Sambamba na hilo Kamanda Mwaibambe amesema hali ya kituoni hapo kwa sasa imetulia baada ya wananchi kufurika kulalamikia mauaji hayo, na kwamba amezungumza na ndugu wa familia kuwaeleza jinsi tukio lilivyokuwa.

Pia Kamanda Mwaibambe amewataka watu kutochukulia tukio hilo kisiasa, isipokuwa ni kama tukio lingine la mauaji, ingawa sio jambo zuri kwa mtu yeyote.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search