Sunday, 8 April 2018

MWANAFUNZI WA CHUO CHA UUGUZI KAHAMA AKUTWA AMEFARIKI NDANI YA KALAVATI MJINI SHINYANGA


Mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Kahama mkoani Shinyanga Henry Mwalongo (48) amekutwa akiwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa ndani ya kalavati umefunikwa mchanga na umeharibika vibaya mjini Shinyanga. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule, mwili wa Henry Mwalongo ambaye ni mkazi wa kata ya Mwasele katika Manispaa ya Shinyanga ulikutwa katika kalavati hilo Aprili 6,2018 majira ya saa 2:45 asubuhi katika eneo la Kambarage mjini Shinyanga. 

Kamanda Haule ameleeza kuwa inakadiriwa kuwa mwili huo ulikuwa ndani ya kalavati kwa muda wa siku tano na sehemu kubwa ya mwili wake ilikuwa imezama kwenye mchanga. 

“Baada ya mahojiano na baadhi ya ndugu za marehemu walieleza kuwa marehemu alikuwa na tabia za kunywa pombe kupindukia 'ulevi wa kupindukia' na hilo lilikuja kujithibitisha baada ya kumkuta akiwa na chupa ya pombe kali katika mfuko wa koti lake alilokuwa amevaa”,amesema Kamanda Haule. 

Hata hivyo amesema chanzo cha kifo hicho bado kinachunguzwa kwani inaonekana kifo chake ni cha mashaka. 

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search