Tuesday, 22 May 2018

AUWA KWA KUCHOMWA MOTO BAADA YA KUTUHUMIWA KUVUNJA DUKA NA KUIBA ELFU 20


Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Kambarage 14 Kata ya Buhahala Mjini Geita wakiwa wanashangaa mwili wa marehemu Erick maarufu kwa jina la 'White' baada ya kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali akidaiwa kuvunja duka na kuiba shilingi 20,000/-.
Wananchi wakiwa wanashangaa tukio hilo.
Duka ambalo alivunja marehemu na kuchukua kiasi cha shilingi 20,000/-
****
Kijana aliyefahamika kwa jina moja la Erick  maarufu "White" mkazi wa Mtaa wa 14 Kambarage Kata ya Buhalahala wilayani Geita ameuawa kisha mwili wake kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali akituhumiwa kuvunja duka la Michael Yusuf na kuiba Shilingi elfu ishirini(20,000/-) .

Hatua hiyo imefikiwa baada ya wananchi kumtuhumu kijana huyo kujihusisha na uhalifu wa mara kwa mara na kwamba kipindi cha nyuma amewahi kuhusika na ubakaji wa mwanamke mwenye umri wa miaka sitini (60).

Baadhi ya wananchi waliofika eneo la tukio wamesema kijana huyo amekuwa na kawaida ya kufanya uhalifu kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuuawa.

“Tunasikitika sana na tabia ya baadhi ya vijana kushindwa kufanya shughuli kwa njia ya halali na kujipatia kipato matokeo yake wamekuwa wakitumia njia za panya kutafuta mafanikio ya haraka jambo ambalo sio sahihi kabisa mimi nisema hatua ambayo wameichukua wananchi sio nzuri ni bora wangeacha nyombo vya usalama vitatue tatizo hili”,alisema Bi,Jamila Hassan.

Baadhi ya wazee wa mtaa huo wamesema vijana wanaojihusisha na uhalifu wamekuwa wakihifadhiwa na mmoja wa wananchi wa eneo hilo.

“Hapa mtaani kuna mkubwa wao ambaye amekuwa akiwatunza vijana hawa ingawa tunamjua ila hatutaki kumsema tumemuhifadhi siku nyingine tutamtaja endapo akiendelea na tabia hizi sisi wazee zinatuchukiza sana”,alisema Mzee Safari Malando.

Mwenyekiti wa mtaa huo Mfaume Nkerebe amesema anamfahamu marehemu kutokana na vitendo vyake vya uhalifu na kwamba tukio hilo sio la kwanza kwani alishawahi kuiba kwenye stationary na kumbaka bibi kizee wa miaka sitini.


Kamanda wa Polisi Mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiwataka wananchi kutokujichukulia sheria mkononi.

Chanzo - Madukaonline blog

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search