Tuesday, 8 May 2018

BINT AUAWA KIKATILI KWA KUKATWA KATWA SEHEMU MBALIMBALI ZA MWILI WAKE IKIWEMO SEHEMU ZA SIRI NA WATU WASIOJULIKANA


Binti anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 14 hadi 16 ameuawa kikatili kwa kukatwa na kitu chenye makali kinachosadikiwa kuwa ni panga na kutenganishwa kiwiliwili na miguu sehemu ya kiuno kisha kuondolewa matiti na sehemu zake za siri katika kata ya Ibadakuli mkoani Shinyanga.

Tukio hilo limetokea Mei 2,2018 majira ya saa sita mchana katika mtaa wa Jilungi kata ya Ibadakuli manispaa ya Shinyanga ambapo vipande vya mwili wa binti huyo vilikutwa kwenye mfuko wa sandarusi uliotupwa kando ya barabara kuu ya Mwanza - Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule,binti huyo asiyefahamika jina wala makazi yake aligundulika akiwa ameuawa na mtu/watu ambao bado hawajafahamika kwa kukatwa na kitu chenye makali.

"Alitenganishwa kiwiliwili na miguu sehemu ya kiuno kisha kuondolewa matiti yake pamoja na sehemu zake za siri na wahusika kuondoka na viungo hivyo",alieleza Kamanda Haule.

"Mwili wa marehemu uligundulika ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi uliotupwa kando kando ya barabara kuu ya Mwanza - Shinyanga eneo ambalo mazingira yanaonesha kuwa siyo mahala hasa ambapo tukio lilifanywa bali ni eneo lingine la mbali lilisilojulikana",alifafanua Kamanda Haule.

Alisema chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na imani za kishirikina na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa hatua za uchunguzi na utambuzi.

Aliongeza kuwa jitihada za kuwabaini,kuwasaka na kuwakamata watu waliohusika katika tukio hilo zinaendelea.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search