Tuesday, 29 May 2018

Diamond Afunguka Kwa Mara ya Kwanza Sakata la Kumwaga Zari

AMEFUNGUKA kwa mara ya kwanza! Baada ya kusambaa kwa maneno ya chinichini kwamba mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amemuangukia mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ akimuomba radhi ili warudiane, staa huyo ameibuka na kutolea ufafanuzi ishu hiyo.

Ubuyu huo uliosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, uliibuka hivi karibuni na kueleza kuwa, kwa nyakati tofauti, Diamond alitinga nchini Afrika Kusini ‘Sauz’, nyumbani kwa mwanamama huyo wa Kiganda na kumuomba msamaha ili waweze kurudiana na kulea watoto wao wawili, Tiffah na Nillan.

ETI NI KWA SABABU KAMKOSEA…

Ubuyu huo ulikolezwa nakshi mitandaoni baada ya kuaminika kuwa, Diamond ndiye mwenye makosa ndiyo maana Zari alitangaza kumuacha.

KWA NINI ZARI ALIMUACHA?

Mara kadhaa Zari amekuwa akieleza wazi kwamba, kilichomsababisha aamue kummwaga Diamond ni kutokana na kutokuwa mwaminifu na kuhisi anamkosea heshima.

MAHOJIANO ‘KARENTI’

Kwenye mahojiano yake ya hivi karibuni ‘karenti’ jijini Nairobi, Kenya, Zari alisema kuwa, aliamua kumpiga chini Diamond kutokana na matendo yake maovu (michepuko) na kamwe hayuko tayari kurudiana naye.Alisema kuwa, ataendelea kubaki kuwa baba wa watoto wake, lakini uhusiano wao hauwezi kufufuka upya kwa sababu ya usalama wake.


TUANGAZIE VYANZO VINGINE

Vyanzo vingine ambavyo vilizungumza na Ijumaa Wikienda viliushibisha zaidi ubuyu wa mkali huyu wa ngoma ya African Beauty kwa kueleza kuwa, Diamond anahaha kunusuru uhusiano wake kwani Zari ndiye mwanamke pekee, chaguo la mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’.

“Hakuwa na jinsi, mama yake hamtaki Mobeto (Hamisa) kama ulivyoona juzikati alimpa vitasa. Mama Diamond kipenzi chake ni Zari hivyo hiyo pia imechangia kumshawishi Diamond aende Sauz kuomba radhi,” kilieleza chanzo kimoja, madai ambayo pia yalielezwa na vyanzo vingine tofauti.

KWA NINI

DIAMOND ANASEMAJE?

Baada ya kupata ubuyu huo kutoka vyanzo mbalimbali, wikiendi iliyopita Ijumaa Wikienda lilimtafuta Diamond ambapo kwa mara ya kwanza tangu aachwe na Zari alimzungumzia mrembo huyo aliyempa heshima ya kuwa baba kwa kumzalia watoto hao wawili kwani kabla ya hapo alisimangwa kutokana na ishu ya kutopata mtoto na msururu wa warembo ‘aliodozi’ nao kimalovee.

AKATAA KUZUNGUMZIA YA KENYA

Kwenye mazungumzo hayo maalum, Diamond alikataa kuzungumzia kauli za Zari alizozitoa hivi karibuni huko Nairobi dhidi yake kwa kile alichodai kuwa hakina maana kwa sasa. “Hayo ya Kenya bwana achana nayo maana yameshapita, mimi nafikiri niulize kuhusu haya ya sasa itapendeza,” alisema Diamond.KUHUSU KUOMBA RADHI SASA…

Alipoulizwa kuhusu madai hayo mapya ya kudaiwa kuenda Sauz mara kadhaa kumuomba radhi mama watoto wake huyo, Diamond alianza kwa kukiri kwenda nyumbani kwa Zari, Sauz kisha akafafanua zaidi madai hayo.

“Ni kweli ninaenda. Siyo mara moja au mara mbili nimeenda. Nakwenda kule si kwa maana ya kumuomba msamaha, hapana. Nakwenda kule kwa ajili ya kuwaona wanangu. “Haiwezekani eti niwe natuma tu fedha kwa ajili ya matumizi halafu nimeenda Sauz, nisiende kuwaona wanangu, hilo litakuwa ni jambo la ajabu sana.

“Hao wanaosema kwamba sijui nimemuangukia, nafikiri itakuwa ni maoni yao tu na stori za kutunga, lakini kimsingi ni kwamba hayana ukweli wowote. “Zari ni mama wa watoto wangu na itabaki kuwa hivyo,” alisema Diamond.

TUMEFIKAJE HAPA

Baada ya kuugulia moyoni kwa muda mrefu, Februari 14, mwaka huu, Zari ‘yalimfika hapa’, akaona isiwe tabu, kupitia ukurasa wake wa Instagram, akatangaza rasmi kummwaga Diamond.

Badala ya kuposti maua yenye kuashiria upendo kwa maana ya kusherehekea sikukuu ya Wapendanao (Valentine’s Day), Zari aliposti ua jeusi na kusindikiza na ujumbe mzito uliobeba hoja za kwa nini ameamua ‘kumtapika’ Diamond.

UJUMBE ULISOMEKA WENYEWE

Kwenye ujumbe huo, Zari, mama wa watoto watano, alisema anatambua kwamba ilikuwa vigumu kwake kufikia umauzi huo, lakini hakuna namna anayoweza kufanya kulinda heshima yake kwani Diamond amekuwa akihusishwa na skendo mbalimbali za wanawake katika vyombo vya habari. Mwisho akapigilia msumari ujumbe wake kwa kusema ameamua kuachana na Diamond kama mpenzi wake, lakini ataendelea kubaki kama baba wa watoto wake.

WANAWAKE WENYEWE NI WAPI?

Licha ya kwamba yapo maovu ambayo yanadaiwa kufanywa kwa siri na Diamond, lakini yaliyoweza kunaswa na mapaparazi na kupamba vyombo vya habari ni pamoja na ishu ya kumpa mimba mwanamitindo Hamisa Mobeto.

Huku akiwa kwenye uhusiano mzito na Zari, Diamond alijiiba kwa siri na kufanikiwa ‘kummega kisela’ Mobeto hadi kuzaa naye mtoto mmoja, hali ambayo inadaiwa kumkasirisha mno Zari. Kama hiyo haitoshi, imedaiwa kuwa madai ya Diamond kurudiana na mrembo Wema Isaac Sepetu nayo yalikuwa yakimkosesha usingizi Zari.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search