Thursday, 10 May 2018

Dodoma: Naibu Spika amtoa nje ya ukumbi wa Bunge Mnyika kwa kutoheshimu kiti cha Spika

FB_IMG_1525880179779.jpg
Naibu Spika Dk. Tulia Ackson ameagiza kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge, mbunge wa Kibamba (CHADEMA), John Mnyika kwa kutoheshimu kiti cha Spika. 

Ametoa agizo hilo leo jioni Mei 9,2018 bungeni Jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19. 

Sakata hilo liliibuka baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kumaliza kuchangia bajeti hiyo na Dk Tulia kumuita Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso kujibu hoja za wabunge zilizoibuka katika mjadala huo. 

Kabla ya Aweso kuanza kuzungumza, Mnyika alisimama akitumia kanuni ya 69(1),kutaka kuahirishwa kuhitimishwa kwa hoja ya Wizara hiyo ili apewe nafasi ya kutoa hoja yake ya kwanini bajeti ya Wizara hiyo isipitishwe na Bunge. 

Mara baada kauli hiyo, Dk Tulia alisimama akitumia kanuni ya 69(2), kusema kama Spika atakuwa na maoni kwamba kuwasilishwa kwa hoja hiyo ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge, atakataa kuitoa ili ijadiliwe. 

Kauli hiyo ilipingwa na Mnyika na wabunge wa upinzani, wakimtaka Dk Tulia ampe nafasi atoe hoja yake.

Kitendo hicho kiliibua mvutano ambapo Naibu Spika alimtaka Mnyika kutulia lakini aligoma akishinikiza kutaka kuruhusiwa kutoa hoja yake. 

Kufuatia kitendo hicho, Dk Tulia alimtaka Mnyika kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, amri ambayo mbunge huyo wa Kibamba aliitii na kusindikizwa na mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA), John Heche. 

Naibu Spika Dk. Tulia Ackson amemtoa ukumbini mbunge wa Bunda Mjini (CHADEMA), Ester Bulaya kwa kutoheshimu kiti cha Spika.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search