Friday, 18 May 2018

IGP AFANYA MABADILIKO KWA MAKAMANDA WA POLISI


Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemteua Naibu Kamishna wa Polisi, Maulid Makabila kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (D/DCI) Zanzibar, huku akifanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.

Kabla ya uteuzi huo, Makabila alikuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia uhalifu makao makuu ya Polisi Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Mei 17, 2018 na msemaji wa polisi, Barnabas Mwakalukwa imeeleza kuwa katika mabadiliko hayo aliyekuwa DCI Zanzibar, Ramadhan Ng’anzi ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Charles Mkumbo aliyehamishiwa makao makuu ya upelelezi, Dar es Salaam.

Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali anakwenda kuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa polisi, Thobias Sedoyeka aliyekuwa makao makuu ya upelelezi Dar es Salaam.

“Kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Unguja, Makarani Khamisi amehamishiwa makao makuu ya upelelezi Zanzibar na nafasi yake kuchukuliwa na kamishna msaidizi wa polisi, Suleiman Hassan aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kaskazini Unguja,” anasema Mwakalukwa katika taarifa hiyo.

Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hasina Ramadhani Taufiq anakuwa ofisa mnadhimu makao makuu ya polisi Zanzibar na nafasi yake inachukuliwa na kamishna msaidizi, Haji Abdallah Haji aliyekuwa ofisa mnadhimu Mkoa wa Mjini Magharibi.

Taarifa hiyo inaeleza mabadiliko hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Chanzo- Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search