Friday, 18 May 2018

IPTL wavurugana, Sethi aibuka na kusisitiza kampuni bado mali yake

[​IMG]
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MWANASHERIA wa mmiliki wa Kampuni ya PAP/IPTL, Harbinder Sing Sethi, Hajra Mungula, ameibuka na kusema Sethi bado Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo.

Pia, amewataka Watanzania kupuuza kwa taarifa zilizotolewa awali na watu wanaojiita kuwa Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo.

Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Hajra alisema yeye kama mwanasheria wa Sethi, amewasiliana na mteja wake, ambaye yuko rumande na kushangazwa na taarifa hizo.

Alisema hivi karibuni kumeripotiwa taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba kampuni inayomilikiwa na Harbinder Sing Sethi imebadilisha uongozi katika ngazi za Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na Mkurugenzi mtendaji wake.

“Taarifa iliyosambazwa na anayejiita mwenyekiti wa bodi mpya, Ambroce Brixio imemtaja yeye kuwa na cheo hicho na Joseph Makandege kuwa Mkurugenzi wake ambaye kwa miezi kadhaa sasa hajawahi kuonana nae ikiwemo hata kutofika mahakamani siku ambazo kesi imekuwa ikitajwa, ilieleza taarifa hiyo.

Hajra, alisema taarifa hizo zimemfikia kwa masikitiko makubwa Mwenyekiti halali na mmiliki wa kampuni hii ya kuzalisha umeme ya IPTL ambayo kimsingi inamilikiwa na kampuni anayoimiliki ya Pan Africa Power Solutions(PAP).

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, alisema pamoja na kuagiza wanasheria wake kuchukua hatua za haraka za kisheria mwenyekiti Sethi pia hana taarifa zozote juu ya mabadiliko hayo.

“Mwenyekiti Sethi anapenda kuutaarifu umma kupitia sisi kwamba wazipuuze taarifa hizo kwa kuwa hazitokani na mamlaka halali za kisheria za kampuni hiyo,” alisema mwanasheria huyo.

Alisema pamoja na kwamba Mwenyekiti Sethi bado yuko mahabusu akituhumiwa mashtaka kadhaa ya jinai, hiyo haiondoi ukweli kuwa IPTL ni kampuni binafsi yenye wamiliki halali wenye hisa halali na wala sio NGO ambayo mtu yeyote anaweza kutangaza mapinduzi ya kiuongozi wakati wowote.

“Mwenyekiti anapenda kuwahakikishia watanzania wote kuwa licha ya uwepo wa mashtaka yanayomkabili bado kampuni hiyo ipo chini ya usimamizi salama wa PAP na kwamba madeni yote, madai, mali na stahiki zote zizohusiana na kampuni hiyo zipo katika mikono salama mpaka sasa,” alisema

Mwanasheria huyo alisema kuwa Mwenyekiti anawahakikishia Watanzania kuwa ataendelea kutoa ushirikiano mahsusi kuhakikisha nchi inajiepusha na hasara zinazotokana na matendo ya aina ya kina Makandege na wenzake ya kukurupuka bila kufuata sheria na taratibu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search