Friday, 25 May 2018

Mbunge wa Tandahimba, Katani ataka Waziri wa Fedha ashughulikiwe na kuchukuliwa hatua kali

Image result for mbunge katani ahmadi katani
Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Ahmadi ameliomba Bunge kuchukua hatua kali dhidi ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa kutokutoa fedha zinazopitishwa na mhimili huo wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali.

Akichangia bajeti ya wizara ya nishati leo bungeni Mei 25, 2018, Katani amesema miradi mingi imekuwa ikishindwa kutekelezwa kwa wizara ya fedha kushindwa kutoa fedha licha ya Bunge kuzipitisha.
Amesema wakandarasi wa Rea wameshindwa kutekeleza usambazaji wa umeme kwa kukosa fedha ambazo zilipitishwa na Bunge huku mawaziri wakinyooshewa vidole kwa makosa ambayo si ya kwao.

Soma Zaidi: Waziri wa Fedha atajwa kukwamisha miradi ya maendeleo
“Fedha zake tunazozisema zimechukuliwa na wizara ya fedha, sisi kama Bunge tunatoa tamko gani au tunachukua hatua gani, kwa nini tunadharauliwa na Serikali, tufike hatua tufanye uamuzi mgumu ili Bunge litambuliwe kuwa ni chombo muhimu,” amesema Katani.

“Sijui wizara ya fedha tufanye jambo gani, tumeona katika kilimo, fedha za korosho hakuna sijui kuna jinsi gani wizara ya fedha,” ameongeza:
Katani amesema hakuna mpinzani nchini si mzalendo au kupinga miradi yenye tija kwa taifa lakini wanayozungumza Serikali inapaswa kuyasikiliza na kuyafanyia kazi.

“Sisi sote ni wazalendo tunachokisema mtumie hekima za pamoja, mawaziri msikilize yanayosemwa, kama haya mnaambiwa katika Stiegler’s Gorge mkubali tunayosema, kwamba tathimini iko wapi, ilifanyika lini, kwa tukisema mnasema sio wazalendo,” amesema Katani na kuongeza:

“Tunaposhauri tunashauri na nia nzuri, hatuna tatizo na CCM, tuna tatizo na matendo ya CCM, tukisema mnaanza kusema nini.”

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Kiza Mayeye amesema mkoa wa Kigoma na Katavi mpaka sasa haijaingia katika gridi ya taifa, “tunaomba muiingize kama mlivyofanya katika mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuweza kufungua fursa za uwekezaji Kigoma kwani ni mkoa wenye fursa nyingi.”

Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search