Thursday, 24 May 2018

MKE AMUUA MME KWA KISA KISA CHAKULA


Sophia Salehe, mkazi wa Kata ya Namiongo, Newala mkoani Mtwara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, kwa tuhuma za kumuua mume wake kwa kumchoma kwa kisu. 

Mauaji hayo yalitokana na ugomvi baina ya mtuhumiwa ambaye inadaiwa kuwa alikataa wito wa mumewe kupika chakula baada ya kutokushiba.

Akizungumzia na Nipashe jana kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya, alisema tukio hilo lilitokea juzi mkoani humo. 

Kwa mujibu wa Mkondya, mwanamume huyo alikufa papo hapo baada ya kuchomwa kisu na mke wake.

Alisema siku ya tukio majira ya saa 1:30 usiku, mwanamke huyo alimwandalia mume wake chakula na kumpatia.

“Kile chakula kilikuwa kidogo, mume wake, Ahmed Salim, alimtaka arudi jikoni kwa ajili ya kupika tena chakula kwa kuwa hakikumtosha. Hapo ndipo palitokea ugomvi wakalumbana na wakaendelea kugombana na mkewe akachukua kisu na kumchoma kifuani,” alisema Kamanda Mkondya.

Kamanda Mkondya alisema Salim alifariki dunia papo hapo baada ya kutokwa na damu nyingi kwenye jeraha.

Aidha, alisema katika tukio hilo wanamshikilia na mwanaume mmoja ambaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini kutokana na uchunguzi unaoendelea.

Alisema wanamshikilia kijana huyo kwa kuwa katika tukio hilo alikuwapo, hivyo watakapopata maelezo yatakayojiridhisha kutohusika ataachiwa.

“Bado huyu kijana tunamhoji ni kwa nini hakutoa msaada wa kuamua ugomvi huo. Hapa tunataka kujua na yeye amehusika au la na kwa huyu mwanamke taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema. 

Aidha, Kamanda alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala kwa ajili ya kusubiri taratibu za mazishi.
Chanzo- NIPASHE

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search