Thursday, 31 May 2018

NATAKA KUZAA-SEHEMU YA KUMI NA SABA

MTUNZI: JENNIFER ALPHONCE
Nilipanga vitu vyangu haraka kwenye kabati na kisha kutoka.“Nitarudi muda si mrefu.” Nilimuaga na kuondoka.
Nilitoka moja kwa moja hadi chumbani kwa kina Frank sikutaka hata kumuambia
kama nimefika. Niligonga mlango na kisha kuingia ndani.
Frank alikuwa na Innocent walikuwa katikati ya majadiliano, waliponiona
walifurahi sana. Nilienda pale alipokuwa amekaa kwenye kiti kwa nyuma yake
nilimkumbatia kutokea nyuma na kisha nikambusu shavuni na baada ya hapo
nikasogea kitandani na kukaa kwani kiti chake kilikuwa karibu sana na kitanda.
“Mambo.”
“Poa, mzima?”
“Mzima sijui wewe.”
“Naona umerudi mama.”
“Eeee nimerudi.”
“Hakuna shida karibu sana.”
“Ahsante.”
Frank alionesha ucheshi wa hali ya juu nilimpenda, alizidi kunivutia kila siku.
“Aaah ngoja niwaache.” Innocent alisema.
“Aaah mwanangu unaenda wapi sasa na hatujamaliza?”
“Nitakuja baadae.” Innocent alisema.
Alinyanyuka akanikonyeza akaachia kicheko na kisha kuondoka, nilicheka tu.
Tulibaki peke yetu.
“Frank nina tatizo.”
“Tatizo gani tena mimi naweza kukusaidia?” Nilicheka kidogo.
“Unafikiri msaada wa aina gani hata mawazo yako ni ya muhimu tena zaidi ya
sana ndiyo ninayohitaji, mimi na Melania tuna ugomvi na sijui kwa nini.”
Alikuna kichwa na kisha akakikumbatia kichwa chake kwa mikono yake.
“Huyu msichana sijui ana matatizo gani, mbona anakuwa na mambo ya ajabu,
kwanza kwanini ananichukia mimi, mimi nimefanya nini.” Aliongea kwa sauti
yake nzuri ya kiume.
“Sijui.”
“Aaah nashindwa kuelewa kabisa, hivyo ndiyo mlikuwa hivyo tangu mwanzo.”
“Mimi na yeye tumejuana tu hapa chuoni nashangaa amebadilika wala hakuwa vile
kila mtu anashangaa.”
“Ok hamna shida, mimi niko tayari kukabiliana naye wala hanitishi.”
“We unasema, mimi nakaa naye chumba kimoja unafikiri nitaishije.”
“Akikusumbua njoo kaa kwangu.”Nilicheka sana.
“Frank acha utani bwana.”
“Mimi nakuambia kweli.”
“Frank nataka tutoke.” Nilimuambia.
“Twende wapi tena.”
“Nataka twende mlimani City.”
“Sijawahi kufika hilo eneo.”
“Twende, jiandae tuondoke.”
“Nijiandae nini sasa na nipo tayari.”
Nilishindwa kujizuia nikajikuta nimecheka, alikuwa amevaa tshirt kubwa refu
ambalo lilikuwa limekaribia kumfikia magotini lilikuwa jeusi na lilikuwa na
nembo flani ivi ambayo nilishindwa kuielewa kifuani. Na chini alikuwa amevaa
suruali ya kitambaa ambayo haikumfika kwenye vifundo vya mguu.
“Badilisha bwana.”
“Au nivae zile za sikukuu.”
“Hahaha Frank jamani sasa si zitapauka.”
Alicheka na kisha alibadili na kuvaa nguo ambazo zilonekana kumpendeza.
Tuliondoka na kuelekea Mlimani City, nilipitia Bank na kuchukua hela kutoka
kwenye akaunti yetu. Mama hakupenda nitumie hela kwenye akaunti yangu binafsi
hivyo alifungua akaunti ya familia ambayo kila mtu alikuwa akichukua hela mimi,
baba na yeye.
Aliniambia bado nilikuwa mdogo sana kumiliki pesa zangu mwenyewe hata hivyo
aliniambia kwamba akaunti yangu ipo tayari na kila mara alikuwa akiweka pesa
kwa ajili ya matumizi yangu ya baadae.
Nilichukua kama kiasi cha laki sita na kisha kuelekea Mlimani City tukiwa na
Frank.
Nilipanga kwenda kumnunulia baadhi ya nguo ambazo angekuwa anazivaa hapo
chuoni.
Tulizunguka maduka mbalimbali kuchagua nguo ambazo zilimpendeza
nilihakikisha kwamba atakapovaa hizo nguo kila mtu ageuze macho yake
kumtazama.
“Utapendeza kweli ila usiibwe tu.” Frank aliinua macho yake akaniangalia.
“Naanzaje.”
Nilicheka tu.
“Kwanini usiibwe.”“Huu ni mziki mnene Sociolah siwezi kuibiwa kirahisirahisi.” Aliongea huku
akitabasamu.
Tulitoka mlimani City na kisha tukaelekea sehemu kupata chakula Fair delight
pembeni ya Mliman City.
“Chakula kitamu.” Aliongea.
Tulipata chakula na baada ya hapo tulirejea mabwenini kwetu Mabibo ilikuwa
kiasi kama saa tatu, nilipitiliza moja kwa moja chumbani kwa Frank hakuna mtu
ambaye alikuwepo chumbani kwake. Alianza kuzijaribu zile nguo ambazo
nilimnunulia siku hiyo.
“Kuna nini kingine unahitaji?”
“Hamna.”
“Hamna, unaona kama simu yako ni nzuri?”
“Nzuri tu inaingia WhatsApp, inaingia Insta sijui wapi.” Aliongea.
Nilijikuta tu nacheka.
“Kama ni nzuri sawa.”
Mama alipiga simu sikupokea.
“Mbona hupokei?”
“Mama huyu nitaongea naye baadae.”
Tuliendelea kuongea maongezi ya hapa na pale tukipiga story mbalimbali hadi
ilipofika saa tano.
“Frank mimi nahisi usingizi nataka kwenda kulala.”
“Ngoja nikusindikize.”
Alinitoa hadi mbele ya mabweni yetu alinibusu kwenye paji la uso na kisha
kuniacha niliingia bwenini kwetu.
Mimi na Melania tulikuwa tukilala vitanda vya chini, Monica na Fetty walikuwa
wakilala vitandanda vya juu.
Niliingia nikakuta Monica akiwa kitandani kwake juu Fetty na Melania walikuwa
mezani.
Sijui walikuwa wakiongea nini au walikuwa wakifanya nini, niliingia, Fetty
alinyanyuka kuja kunikumbatia Melania alimvuta mkono na kumkalisha kwenye
kiti.
“Unaenda wapi?” Alimuuliza.
Kwa kweli sikuwahi kumshuhudia Melania akiwa katika hali kama hiyo, hali hiyo
ilinifanya nimjue Melania ni mafia kwa maana ile sauti yake ya upole ilibadilika.Fetty hakuwa na jinsi alirudi kitini na kukaa nilicheka kwa upole kiasi kwamba
Melania asingeweza kunisikia.
“Hi..” Nilisalimia.
Aliitikia Monica nadhani Fetty aliogopa kuitikia.
Niliingia kitandani kwangu na kisha kujilaza.
Asubuhi ya siku iliyofuata tulikuwa tuna kipindi cha saa mbili asubuhi niliamka
niliwakuta tayari wote wameshaamka nilielekea bafuni kuoga na baada ya hapo
nilirudi chumabani kwangu kujianda. Walitoka dakika tano kabla yangu, tulipanda
wote gari moja hadi chuoni.
Tulishuka na kisha kuelekea yalipo madarasa yetu, walikuwa hatua zisizopungua
kumi na tano mbele yangu.
Melania akiwa na baadhi ya watu wa darasa letu.Tulipofika karibu na madarasa
yetu kila mtu alikuwa akishangaa.
Nilishindwa kujua kuna nini.
Lakini ghafla nilimuona Melania akisita, mshangao alioupata sikuwahi kumuona
nao hata siku moja.
Ilinibidi kuwa mdadisi ni nini kinatokea na nini kilichomfanya Melania
akashangaa kiasi hiko.
Hakika Frank alikuwa amependeza tofauti na hata vile alivyokuwa akizijaribu zile
nguo. Kitu pekee nilichokijua ni kwamba Frank alikuwa mbunifu sana ila alikuwa
akishindwa kupata mavazi mazuri. Nilimnunulia nguo katika pea lakini alijua
kuchagua nguo zinazoendana hakika alipendeza sana.
Melania alikuwa mbele yangu nilitazama jinsi watu walivyokuwa wakimshangaa
Frank kila mtu akitamani kupiga naye picha, alionekana ni mwanaume wa kileo
ambaye kila msichana angetamani kuwa naye. Niliachia tu tabasamu na kisha
kuongeza hatua zangu, nilimpita Melania kwa hatua za pole pole nilipita mahali
ambapo Frank alikuwa amesimama na kisha kuingia darasani.
“Basi basi inatosha.” Frank alisema na kisha akaniungia tela nyuma yangu.
“Sociolah...” Niligeuka na kumtazama na kisha nikaendelea kupiga hatua hadi
kwenye sehemu ambayo nilizoea kukaa mara zote.
Hata hivyo nilikuta vitu ambavyo vilionesha kuna mtu tayari ameshakaa. Viti
vyote vya mbele vilikuwa vimewahiwa kitu ambacho siyo kawaida mara zote
nilizoea kukaa mbele na hakuna mtu ambaye alikuwa anaweza kukaa kwenye kiti
ambacho nilikuwa nakaa.
“It is yours.” Alisema Frank.“Frank.” Nilimuita.
Watu walianza kuingia darasani nilinyanyua vile vitu na kugundua kwamba
havikuwa ni madaftari. Nilikaa, alikuja kukaa pembeni yangu.
Zilikuwa ni bahasha mbili nilichungulia ndani ya bahasha moja nikakuta kadi nzuri
sana niliifunga bahasha na kisha kuweka kwenye begi langu nikamgeukia Frank.
“Mwalimu ameingia.” Aliniambia, nilicheka tu na kisha kumtazama mwalimu.
Mwalimu alivyoingia tu alimuita Frank.
“Franklin Kazimana.” Aliita.
Frank alisimama.
“Baada ya kipindi uje ofisini kwangu na Cr nitahitaji kukuona baada ya kipindi.”
Watu wote walicheka darasani.
“Mnacheka nini?” Aliuliza mwalimu yule ambaye alikuwa ametuzoea wanafunzi
wake.
“Hamna kitu.” Alituangalia tu na kisha kuendelea.
Mara baada ya kipindi.
“Frank twende.” Nilimuita tulinyanyuka kwa hatua za polepole kuelekea ofisini
kwa mwalimu.
Tulifika ofisini kwa mwalimu.
Mwalimu yule alikuwa akituangalia tu.
“Frank nataka niwape kazi ya kufanya kuna mashindano ya madaktari wanafunzi
kutoka vyuo mbali mbali nataka mkashiriki lakini wewe pekee ambaye
ninakuamini nataka ukatuwakilishe Frank.” Daktari aliongea.
Daktari Kiseyeye alionekana kuwa makini sana.
Frank aliniangalia.
“Hamna shida, yanahusiana na nini?”
“Nitakuja kukupa maelezo kwa njia ya maandishi ilimradi umekubali hakuna
shida.”
“Sawa.”
“Sociolah nataka uwatangazie test watu wako, wiki ijayo kutakuwa na mtihani
wajiandae nitatoa kwenye module ya kwanza niliyofundisha.”
“Sawa mwalimu.”
“Kitu kingine nataka kujua kwanini watu walicheka darasani baada ya kuita
Sociolah?”
Nilitabasamu na kisha nikamuangalia Frank.
“Hapana sijui mimi, ni bora tu ungewauliza wenyewe.”“Hamna shida mnaweza mkaenda.”
Tulitoka tulishikana mikono tukitembea mpaka mgahawani kwa ajili ya kupata
chai.
“Leo tutakunywa chai pamoja.” Nilimuambia.
“Hakuna shida.”
Aliagiza yeye chai mimi niliagiza juisi.
“Kunywa chai Sociolah.”
“Aaah, mimi sipendi sana kunywa chai ujue.”
“Shauri yako mwili haujengwi kwa matofali.”
“Hahaha kama juisi ni matofali sawa.”
Tuliendelea na mazungumzo ya hapa na pale tukifurahia na kucheka.
Nilipopiga jicho pembeni yangu niliweza kumuona Melania akituangalia kwa jicho
kali, nilikatiza tabasamu langu usoni na kisha kubaki nikimshangaa alinyanyuka
ghafla na kuondoka.
Kila mtu mule mgahawani alishangaa hakuna aliyejua sababu yake na mimi
niliamua kumpotezea na kuendelea kuongea na Frank kana kwamba sikumuona.
Tuliendelea na vipindi hadi vilipoisha.........

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search