Wednesday, 16 May 2018

NDOA YA AINA YAKE YAFUNGWA HUKO MKOANI LINDI


Bahati Ramadhani akiwa amembeba mumewe Jivunie Mbunda katika harusi yao iliyofanyika mwishoni mwa wiki. Picha na Jackline Masinde 
**

Ndoa ya Jivunie Mbunda na Bahati Ramadhani inadhihirisha usemi usemao ‘mapenzi sawa na majani huota popote.”


Wawili hao walifunga ndoa juzi mjini Liwale mkoani Lindi na kuvuta hisia za wengi.


Mbunda (35) mwenye ulemavu uliosababisha kuwa na kimo kifupi alifunga pingu za maisha na Bahati (25), mkazi wa Newala mkoani Mtwara aliyemzidi mumewe urefu kama mara tatu hivi.


Ndoa hiyo ilifungwa saa saba mchana katika msikiti wa Mangindi na kukusanya watu wengi huku baadhi wakisimama barabarani wakati bwana na bibi harusi wakitoka msikitini kuelekea nyumbani.


Madereva wa bodaboda hawakuwa nyuma, waliongoza msafara wa maharusi hao huku wakipiga honi.


Nderemo na vifijo vilitawala mtaani, kina mama waliimba nyimbo kumpongeza Mbunda kwa kuoa wakiimba, “Jivu (Jivunie) kaka yetu kaoa,” na wengine wakiitikia wakisema “kaoa.”


Msafara ulipofika nyumbani, ndugu na majirani walitandika kanga na vitenge kwa ajili ya maharusi kupita baada ya kushuka kwenye gari aina ya Toyota Altezza.


Kutokana na hali ya ulemavu ya Mbunda inayosababisha asiweze kutembea, mshenga wake Ismail Mandepe alimshusha kwenye gari na kumketisha kwenye kanga na vitenge na kuibua shangwe huku wananchi waliokuwepo wakisukumana kila mmoja akitaka kuona na kujua kinachoendelea.


Muda mchache baadaye alishuka bibi harusi na kwenda kuketi pembeni kwa mumewe. Kitendo hicho kilisababisha vurugu baadhi ya waliohudhuria wakihangaika kupiga picha.


Tahiba Makingito, mama mzazi wa Mbunda akiongozana na ndugu zake alimpokea na kufanya taratibu za mila.


Baadaye Bahati alimbeba mumewe mithili ya mtoto mchanga na kwenda kuketi naye eneo maalumu lililoandaliwa kwa ajili yao.
Jinsi walivyokutana


Wakizungumza na Mwananchi, wanandoa hao wanasema walikutana baada ya kuunganishwa na ndugu wa Mbunda.


Mbunda anasimulia kwamba, nduguye huyo alimweleza kwamba kuna msichana yuko Newala anayefaa kuwa mke wake.


Alimjibu ndugu yake huyo kuwa kama ni kweli ampatie simu wazungumze.


Mbunda alisema walipozungumza Bahati alikubali, lakini alihitaji kuonana naye kwanza.


“Nilimtumia nauli akaja hapa nyumbani akaniona, basi mwenyewe akaridhia kwa moyo kuwa amekubali kuolewa nami,” alisema Mbunda.


Bahati alisema hajalazimishwa au kushurutishwa na mtu bali amempenda Mbunda kwa moyo wote kwa kuwa hata yeye ni binadamu kama walivyo wengine.


“Nampenda mume wangu, sijalazimishwa na mtu nimeamua mwenyewe,” alisema Bahati.


Shabani Mbaallu, baba mzazi wa Bahati alisema ameridhia kwa mikono miwili binti yake kuolewa na Mbunda.


“Binti yangu alikuja akaniambia amepata mume, lakini ni mlemavu. Nikasema kama umempenda mwanangu sina shida yoyote nakuruhusu ila tu ukamuheshimu mumeo na kumtunza,” alisema.


Salama (22), dada wa Mbunda ambaye pia ni mlemavu alisema hakuamini kama kaka yake angepata mke kutokana na hali yake.


Alisema Mbunda alishapata mwanamke akazaa naye lakini akakataa kuolewa kutokana na ulemavu.


Jivunie Mbunda ni mtoto wa pili kati ya watoto saba wa familia ya Mbunda na kati yao watatu ni wenye ulemavu.


Mwaka 2007 Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwajengea nyumba baada ya vyombo vya habari kuripoti kuhusu kutengwa na kutelekezwa mama mzazi wa Jivunie na watoto wake kutokana na kuzaa wenye ulemavu.
Na Jackline Masinde, Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search