Wednesday, 16 May 2018

RC Morogoro awashtukiza wafanyabiashara,

Na Andrew
Chimesela - Morogoro
Image may contain: 2 people, people standing
Image may contain: one or more people and people standing
Image may contain: 2 people
Image may contain: one or more people and people standing
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Kebwe Stephen Kebwe amefanya ziara ya Kushtukiza na kupita kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta ya kula na sukari katika Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kukagua wafanyabiashara wanaofinya bidhaa hiyo.
Dk. Kebwe amefanya Ziara hiyo Mei 15, mwaka huu akiambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo na kujionea mwenyewe maghala mengi yakiwa yamejaa mafuta ya kula na sukari na kuwataka wafanyabiashara hao kutoficha bidhaa hizo badala yake wazipeleke sokoni kwa ajili ya kuuza kwa wananchi kwa bei elekezi ya Serikali.
Hata hivyo Dk. Kebwe amekemea vikali kitendo cha baadhi ya Wafanyabiashara hao kuchanganya bidhaa za chakula kama mafuta ya kula, sukari na unga na bidhaa nyingine kama sabuni kwa kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha Afya za wananchi.
Katika zoezi hilo la ukaguzi Dkt. Kebwe ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, amemuagiza Kamada wa Polisi wa Mkoa pamoja na Maafisa wa TRA wa Mkoa huo kumchukua na kumhoji Mfanyabiashara maarufu wa Mafuta ya kula Hussein Bionzo na kuzipitia nyaraka zake za biashara hiyo ili kujiridhisha endapo analipa kodi stahiki ya Serikali ama la.
Hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa ya kumtaka Mfanyabiashara huyo kufika kituo cha Polisi na Kuhojiwa imekuja baada ya makosa kadhaa yaliyojitokeza wakati wa zoezi la kukagua bidhaa ya mafuta ya kula katika maghala yake.
Katika Hatua nyingine Dk. Kebwe amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuhusu bidhaa ya Mafuta ya kula kuwa amejionea mwenyewe mafuta hayo yapo ya kutosha na yatauzwa kwa bei ya kawaida.
Hata hivyo, amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa huo kusimamia mafuta hayo kwenye maduka ya reja reja ili yauzwe kwa bei elekezi kwani amesema huko ndiko kuna tatizo la kupandisha kiholela bei ya bidhaa hiyo hususan katika kipindi hiki cha ramadhani.
Hatua ya Dkt. Kebwe kufanya ziara hiyo ya kushtukiza ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutaka kuwachukulia hatua za kisheria watakaoficha mafuta hayo ya kupikia.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search