Wednesday, 2 May 2018

TRUMP ALIJITUNGIA BARUA YAKE KUHUSU AFYA YAKE -DAKTARI

Aliyekuwa daktari wa Donald Trump amesema kwamba si yeye aliyeiandika barua iliyomweleza mgombea huyo wa chama cha Republican wakati huo kuwa aliyekuwa na "afya nzuri ajabu", vyombo vya habari Marekani vinasema.

"[Trump] alitunga na kuamrisha kuandika kwa barua yote," Harold Bornstein aliambia runinga ya CNN Jumanne.

Ikulu ya White House haijazungumzia tuhuma hizo za daktari huyo.

Bw Bornstein pia amesema maafisa wa serikali walitekeleza "uvamizi" katika afisi zake Februari 2017 na kuondoa nyaraka zote zilizohusiana na taarifa za kimatibabu za Bw Trump.

Katika mahojiano na CNN, Bw Bornstein amesema barua hiyo ya mwaka 2015 iliyodokeza kwamba Bw Trump angekuwa "mtu mwenye afya bora zaidi aliyewahi kuchaguliwa kuwa rais" haikuwa utathmini wake wa kitaalamu wa hali yake ya afya.

Barua hiyo ilisema nini?
Barua hiyo ilikuwa na miongoni mwa mengine tamko kuhusu nguvu za kimwili za Bw Trump na ukakamavu wake, ambavyo vilielezwa kuwa "vya kipekee".

Vipimo kuhusu shinikizo la damu yake na pia uchunguzi mwingine wa maabara vilielezwa kuwa "vya kushangaza kwa uzuri wake" na kwamba alikuwa amepoteza uzani wa kilo 7 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Barua hiyo iliongeza kwamba Bw Trump hakuwa na aina yoyote ya saratani na hajawahi kufanyia upasuaji wowote wa maungo.

Wiki kadha kabla ya kutolewa kwake, Bw Trump alikuwa ameandika kwenye Twitter kwamba barua ya kimatibabu ya Bw Bornstein ingeonesha hana kasoro.


"Nina bahati sana kwamba nilibarikiwa na vinasaba vizuri sana," Bw Trump, ambaye ndiye mtu aliyechaguliwa kuwa rais akiwa na umri mkubwa zaidi Marekani, aliandika kwenye Facebook wakati huo.

Januari mwaka huu, Bw Trump alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ambao ulidumu saa tatu kuhusu afya yake ya kiakili.

Daktari wake wa White House Ronny Jackson alisema wakati huo kwamba: "Sina wasiwasi wowote kuhusu uwezo wake wa kufahamu, kufikiria na kuelewa mambo."

Uvamizi wa afisi ya Bornstein ulihusu nini?
Daktari huyo mwenye makao yake New York City anasema walinzi wa kibinafsi wa Bw Trump walifika katika afisi zake New York wakiandamana na wanaume wengine wawili mnamo tarehe 3 Februari 2017.

"Walikaa hapa kwa dakika 25 au 30 hivi, walizua vurugu sana," Bornstein aliambia NBC News, na kuongeza kwamba kisa hicho kilimfanya kujihisi kama "aliyebakwa, kuwa na hofu sana na masikitiko na huzuni."

Anasema nakala halisi ambayo ndiyo pekee aliyokuwa nayo ya rekodi ya afya ya Trump, ikiwa ni pamoja na ripoti za uchunguzi wa maabara, vyote vilitwaliwa na walinzi hao wa Trump.

Kisa hicho kilitokea muda mfupi baada ya gazeti la The New York Times kuchapisha taarifa ambapo Bw Bornstein alisema alikuwa amempendekezea Trump danywe dawa ya Propecia, ambayo ni ya kuzuia upara.

Afisa wa habari wa White House Sarah Sanders baadaye alisisitiza kwamba kisa hicho hakikuwa uvamizi bali lilikuwa tukio la kawaida kwa kitengo cha matibabu cha ikulu ya White House kuchukua umiliki wa nyaraka zote za kimatibabu za rais wa Marekani.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search