Wednesday, 30 May 2018

Waziri, wanasaikolojia wazungumzia kukithiri matukio ya watu kujiuaKwa kawaida binadamu hukiogopa kifo, lakini maswali huibuka pale anapoamua kujitoa uhai.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya watu kujiua, ambapo ndani ya mwezi mmoja, wanne wameripotiwa kujitoa uhai nchini.
Katika tukio la jana, mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Kakonko, mkoani Kigoma, Mejo Banikira (43) alikutwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia taulo.
Kabla ya tukio la Banikira, Mei 6, mwanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Kahororo iliyopo wilayani Bukoba, Robert Masaba alijinyonga zikiwa zimesalia saa chache kabla ya kufanya mtihani wa mwisho.
Siku nne baadaye mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Makumira mkoani Arusha, Luciana Richard (25), mkazi wa Morogoro alijinyonga akiwa chumbani kwake kwa kile kilichodaiwa kuwa ni msongo wa mawazo.
Tukio hilo lilitokea katika Kitongoji cha Kilalanaiti, Kijiji cha Ndatu, Kata ya Pori. Mwanafunzi huyo alijinyonga kwa kutumia mtandio alioufunga juu ya mlango wa bafu.
Mei 27, 2018, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St Augustine (Saut) tawi la Mbeya, Moses Mashaka alikutwa amekufa ikidaiwa alijinyonga chumbani kwa kutumia shuka.
Wakati matukio hayo yakiendelea kujitokeza, Januari ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), iliitaja Tanzania kushika nafasi ya 27 barani Afrika kwa vifo vinavyotokana na watu kujiua.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, ripoti hiyo inaonyesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wanaojiua.
Katika ukanda huo, Rwanda inaongoza kwa kuwa na asilimia 8.5 ya vifo vya kujiua ikifuatiwa na Burundi yenye asilimia nane.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Uganda kwa kuwa na asilimia 7.1 huku Tanzania ikishikilia nafasi ya nne kwa kuwa na asilimia saba.
Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alitaja chanzo cha matukio hayo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii wa kukabiliana na msongo wa mawazo hatua inayosababisha baadhi ya watu kuchukuliwa hatua za kisheria kwa makosa ya majaribio ya kujiua.
“Kabla ya kuchukua uamuzi huo ziko hatua, eneo mojawapo ni sonona (depression), hii ni hatua inayosumbua wengi kwa mfano huzuni ya kwenye mgogoro wa mapenzi na kwa bahati mbaya (mtu) asipate mshauri wa karibu,”alisema.
Dk Ndugulile alisema idadi ndogo ya watalaamu wa saikolojia nchini ni sehemu ya changamoto ya jamii kukosa msaada wa ushauri na Serikali inahitaji kuongeza nguvu zaidi katika kushughulikia wagonjwa wa sonona.
Wanasaikolojia wanasemaje?
Wanasaikolojia wanasema binadamu hufikia hatua ya kujiua baada ya akili kukosa uwezo wa kuhimili uzito wa changamoto anazokabiliana nazo.
Mwanasaikolojia Charles Nduku alisema maeneo mawili yanayochagiza kuwapo kwa idadi kubwa ya vifo vya aina hiyo ni kutotimiza malengo na matarajio ambayo mtu hujiwekea pamoja na presha za kimaisha kuzidi uwezo wa kufikiri.
Nduku alisema uamuzi huo hutokea dakika chache baada ya mtu kukutana na changamoto inayozidi uwezo wake wa kupata mbadala. Alisema akili ya mtu anayetaka kutekeleza tukio hilo kwa wakati huo huwa imefungiwa katika suluhisho hilo pekee kama njia ya kuyakimbia matatizo.
“Asili ya tatizo liwe kubwa au dogo halimfanyi mtu kujiua ila uwezo wake wa kuhimili tatizo hilo, anajiuliza kwa nini mimi, kwa nini nisife tu? Sasa ukimuwahi dakika tano kabla ya kufanya uamuzi huo ukamwambia kuwa yeye ni wa thamani, anaweza kubadili uamuzi huo palepale,” alisema.
“Mara nyingi matukio ya kujiua yanahusisha kundi la mapenzi kwa sababu watu wanaishi kwa hisia zaidi, lakini ukikuta anayeishi kwa kutafakari siyo rahisi kuchukua uamuzi huo.”
Kwa bara la Afrika, Equatorial Guinea inaongoza kwa wingi wa vifo vinavyotokana na watu kujiua kwa kuwa na asilimia 22.6 ikifuatiwa na Angola yenye asilimia 20.5 na ya tatu ni Ivory Coast yenye asilimia 18.1.
Mwanafunzi, daktari
Mwanafunzi wa Saut alijiua kwa kujinyonga na shuka chumbani kwake katika mtaa wa Maendeleomjini Mbeya.
Mshauri wa wanafunzi chuoni hapo, Daud Kapufi alisema baada ya uchunguzi wa daktari, polisi walitoa ruhusa kwa familia kuuchukua mwili. Mwili huo umesafirishwa kuelekea Geita kwa mazishi.
Naye Dk Banikira alikutwa amejinyonga chumbani kwake akiwa na miezi isiyozidi minane tangu alipohamishiwa Kakonko kutokea Simanjiro.

Kwa mujibu wa majirani, mtaalamu huyo wa afya alikuwa akiishi peke yake katika makazi hayo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search